WANANCHI wa kijiji cha Mapogolo Kapunga
kata ya Itamboleo Wilaya ya Mbarali mkoani hapa wamekataa kupokea majengo ya
Shule yaMsingi iliyojengwa na Mwekezaji wa Shamba la Kapunga Rice Project
kutokana na kutokuwa na mahusiano mazuri.
Wakizungumza katika Mkutano wa hadhara kijijini
hapo baada ya Mwenyekiti wa kijiji hicho Ndugu Ramadhani Nyoni kutoa taarifa
Kwa Mkuu wa Wilaya hiyo Gulam Husein Kiffu juu ya kukamilika kwa ujenzi wa
shule hiyo iliyojengwa na Mwekezaji Kilomita 8 kutoka katika makazi ya watu.
Kutokana na kukamilika kwa majengo hayo Mkuu wa
Wilaya kupitia Mkutano alioufanya Aprili 25 na Serikali ya Kijiji aliwasihi
wananchi kuipokea Shule hiyo ikiwa ni pamoja na kuwahamisha wanafunzi wanaosoma
katika Shule ya Msingi Kapunga na kuhamia Katika shule mpya ifikapo Mei 3 Mwaka
huu.
Lengo la kujengewa shule nyingine ni kutokana na
Mwekezaji kutaka Wananchi wampishe katika eneo lake hivyo akalazimika kujenga
Shule nyingine ambayo baada ya kukamilika Wananchi wameikataa kutokana na
kutokuwa na mahusiano mazuri kati ya Mwekezaji na Wananchi wanaoyazunguka
mashamba.
Aidha wakizungumzia sababu za kukataa kupokea
Majengo hayo Viongozi wa Serikali ya Kijiji wamesema tangu ujenzi uanze
hawajawahi kupewa taarifa ya aina yoyote, pia umbali mrefu kutoka maeneo
wanayoishi na Shule mpya ilipojengwa ambao ni Kilomita Nane.
Sababu nyingine wamedai kutokuwa na imani na
Mwekezaji huyo kutokana na kuwa na tabia ya kuwanyanyasa Walimu ambao awali
amewahi kuwafukuza katika majengo ya Shule hali iliyopelekea Walimu hao
kutembea umbali mrefu kwenda Shuleni kufundisha.
Akitoa taarifa kwa wananchi katika Mkutano wa
hadhara uliofanyika Aprili 29, Mwaka huu Ofisa Mtendaji wa Kijiji Ndugu Peter
Kita amesema Mwekezaji alitoa taarifa kwa Mkuu wa Wilaya kuhusu kukamilika kwa
ujenzi na kuomba kuwakabidhi ili waanze kuyatumia lakini Wananchi
hawakukubaliana naye.
Wananchi hao wamefafanua kuwa wao hawako
tayari kupokea majengo ya shule hiyo kutokana na Mwekezaji kutokuwa na msaada
wowote katika kijiji ikiwemo Shughuli za Kijamii kama Maji , Afya, Barabara na
Umeme.
Wamesema kwa sasa wako tayari kujenga Shule yao
kwa nguvu zao ambapo walisema tayari wameshapata kibali na michoro kutoka Ofisi
ya Mkurugenzi wa Wilaya ya Mbarali.
Wameongeza kuwa sababu zingine za kukataa mradi
huo ni kuhofia usalama wa wanafunzi kutokana na kuwepo kwa mfereji mkubwa wa
maji karibu na Shule ilipojengwa pamoja na ubora wa majengo kuwa hayataweza
kuhimili vishindo vya wanafunzi zaidi ya 700.
Mbali na Ajenda ya Shule wanakijiji hao pia
walikuwa wakisomewa taarifa ya mapato na matumizi ya kijiji ambapo pia
waliidhinisha bajeti ya kipindi cha Mwaka 2013/2014 zaidi ya Shilingi Milioni
130 zitakazokusanywa kutokana na vyanzo mbali mbali.
Mikakati ya ujenzi wa Shule yao mpya ulianza
hapo hapo ambapo zaidi ya Shilingi 90,000/= zilikusanywa na kuazimia kila kaya
kuchangia Shilingi 20,000/= hadi ifikapo Mei 15, Mwaka huu ambapo
wanatarajiwa kukusanya zaidi ya Milioni Kumi.
Aidha wametoa wito kwa mwekezaji kutowasumbua
wanafunzi wanaosoma darasa la nne na darasa la saba kutokana na kuwa na
mitihani ya kitaifa ambapo walisema Shule yao mpya inatarajiwa kukamilika
katika muda mfupi baada ya kukamilisha maandalizi yote.
Haya hivyo ikumbukwe kuwa Mwekezaji huyo wa
Kapunga Rice Project bado anakesi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya
akituhumiwa kuteketeza mazao ya wananchi kwa sumu na kuwasababishia hasara na
madhara wananchi.
Na Mbeya yetu
|
0 comments:
Post a Comment