Vyombo vya habari nchini vimetakiwa kutumia nafasi na taaluma maalum iliyonayo kuhakikisha kuwa umaskini unapigwa vita kupitia sekta ya kilimo.
Wito huu umetolewa wakati wa semina ya mafunzo kwa waandishi wa habari kuhusiana na uandishi wa habari za biashara na uchumi.
Pia semina hiyo ililenga kuwapa uwezo na uelewa wa kuandika kuhusu matokeo ya utafiti kuhusu ripoti inayojulikana kama AgFiMS Tanzania 2011 Demand Side Technical Report.
Ripoti hiyo ilifanywa na Financial Sector Deepening Trust Tanzania (FSDT).
Mkuu wa kitengo, Huduma za Kifedha sekta ya kilimo, FSDT, Bw. Mwallu Mwachang’a alisema jana jijini Dar es Salaam kwamba vyombo vya habari vina nafasi ya pekee kutafuta, kuchambua na kusambaza habari kuhusiana na maswala ya fedha na kilimo kuliko taaluma nyingine yoyote na kwamba ni vyema kama wakitumia nafasi hiyo kuendeleza sekta ya kilimo na hivyo nchi nzima kwa ujumla.
“Waandishi wana nafasi muhimu na kipekee katika kuripoti maswala ya mahitaji ya fedha katika sekta ya kilimo…nia yetu ni kuwawezesha kufanya hivyo,” alisema.
Mmoja wa wawezeshaji katika mafunzo hayo toka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. Humphrey Moshi alisema huu ni muda muafaka kwa waandishi wa habari nchini kutumia taaluma yao kuokoa sekta ya kilimo, hasa upatikanaji wa fedha kwa wakulima.
“Fursa za fedha kwa sekta ya kilimo inayoajiri watu wengi hasa vijijini bado ni changamoto kubwa, hili ni tatizo na waandishi wana nafasi kushughulikia changamoto hii,” alisema Prof. Moshi.
Mkurugenzi wa maswala ya ufundi, FSDT, Mr. Sosthenes Kewe alisema moja ya vikwazo vinavyowakabili wakulima wadogo na wanaojihusisha na biashara ya kilimo ni ukosefu wa fedha kwa kuwa vyombo vya fedha bado vinawaona kama watu wasiokua na sifa kupata mikopo.
“Hili limesababisha vyombo hivi vya fedha kutokua na huduma zinazolenga maendeleo ya kilimo kwa kiwango kinachotakiwa,” alisema.
Moja ya madhumuni ya ripoti ya AgFiMS Tanzania 2011 ilikua ni kusaidia maendeleo ya huduma za fedha kuchochea biashara katika kilimo na kufikisha huduma hizo kwa wakulima.
Kwa mujibu wa wataalamu, maendeleo ya kilimo ni njia bora ya kupunguza umaskini. Asilimia 75 ya maskini katika nchi zinazoendelea wanaishi vijijini na asilimia 85 ya watu hao wanategemea kilimo kuendesha maisha yao.
FSDT inalenga kuhamasisha watu katika kada na maeneo mbalimbali nchini kukubalika na kushiriki kwa kiwango kinachoridhisha katika mfumo rasmi wa kifedha.
michuzi
michuzi
0 comments:
Post a Comment