KAMPUNI
ya bia Tanzania (TBL) kupitia bia yake ya Kilimanjaro Premium Lager,
inaendelea na tamasha kubwa la muziki lijulikanalo kama ‘Kili Music Tour
2013’ wikiendi hii mjini Tanga.
Tamasha hili kubwa litafanyika Jumamosi tarehe 29 Juni, 2013 mjini Tanga kwenye kiwanja cha
Mkwakwani na litajumuisha wasaniii 8 ambao ni Ally Kiba, Snura Mushi,
Professor J, Mwana FA, Recho, Mzee Yusuph, Roma na Kala Jeremiah.
Tamasha
hili ambalo hapo awali lilikuwa linajulikana kama KTMA Winners Tour
mwaka huu lilibadilishwa jina na kuwa Kili Music Tour ili kupanua wigo
wake na kujumuisha wasanii walioshinda tuzo za Kili Tanzania Music
Awards, wasanii waliopendekezwa kwenye tuzo na wasanii ambao
hawakushiriki kwenye tuzo lakini ni vinara kwenye tasnia ya muziki
nchini.
Meneja
wa bia ya Kilimanjaro Premium Lager Bwana George Kavishe alinukuliwa
akisema “tumeona ni jinsi gani mkoa wa Dodoma uliitikia wito na
kushiriki kwa kikamilifu kwenye Kili Music Tour wikiendi iliyopita,
hivyo basi tunategemea Tanga itajumuika nasi ipasavyo kufanikisha
tamasha litakalofanyika mkoani hapo Jumamosi ya tarehe 29.”
Bwana
Kavishe aliendelea kufafanua kuwa “mwaka huu ndani ya staili ya
“kikwetu kwetu” bia ya Kilimanjaro Premium Lager inahakikisha kuwa kama
kawaida inatoa bonge la kiburudisho kwa watanzania ikizingatia jinsi
watanzania tunavyojivunia mambo yetu ya kitofauti kama muziki wetu wa
bongo fleva, dansi yetu ya kiduku, kandanda letu lenye ushabiki wa simba
na yanga, lugha yetu ya kipekee na bia yetu ya Kilimanjaro
iliyotengenezwa Tanzania, kwa kutumia viungo vya kitanzania na
watanzania.”
Msanii
aliyebobea wa bongo flava ajulikanaye kama Professor J (Joseph Haule)
naye alisema “wakazi wa Tanga na vitongoji vyake wasubiri shoo kubwa ya
kufana kama waliyoipata wakazi wa Dodoma wiki iliyopita. Tunategemea
kuwashangaza wanatanga kwa kuwapa vionjo ambayo hawajawahi kuviona kwani
mimi na wasanii wenzangu tumejipanga kikamilifu kuhakikisha kuwa
hatuwaangushi mashabiki wetu na kuwa tutawapa bonge la kiburudisho!”
0 comments:
Post a Comment