Main Menu

Friday, March 29, 2013

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA DR. ABDALA KIGODA AZOMEWA MKOANI MTWARA

Wananchi wa mkoa wa Mtwara wa kusini mwa Tanzania, jana waliwazomea Mawaziri wawili wa serikali ya Rais Jakaya Kikwete, jambo lililowafanya mawaziri hao na mgeni wao balozi wa Nigeria kukatiza mkutano wao. 

Mawaziri hao ambao ni Dk. Abdallah Kigoda wa Wizara ya Viwanda na Biashara na Naibu Waziri wa Uchukuzi, Charles Tizeba, walikuwa wameongozana na Balozi wa Nigeria nchini Tanzania, Nshaya Manjabu, na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Dangote ya Nigeria, Deva Kumar. 

Tukio hilo limekuja zikiwa zimepita wiki chache tu tangu kutokea kwa vurugu kubwa mkoani humo ambapo wananchi waliharibu mali za baadhi ya viongozi wa kisiasa na kiserikali na kumuua askari mmoja huku watu wengine wanne wakiuawa kwa kupigwa risasi. 

Wananchi wa Mtwara na Lindi wamekuwa na msimamo mkali kuhusu suala la gesi na wamekuwa wakipinga serikali kutaka kupeleka gesi ya maeneo hayo jijini Dar es Salaam bila ya watu wa maeneo hayo kufaidika na gesi hiyo. 


Taarifa zinasema kuwa, mara baada ya mawaziri hao kufika mkutanoni, Waziri Kigoda aliwasalimia wananchi akisema: "Mtwara oyeee!!!" Waziri huyo aliitikiwa na wananchi: "Haitoki hata kama umekuja wewe hatutaki wala hatukuelewi! Mlikuwa wapi kuja huku mapema kutuelewesha habari za viwanda?" Wakati purukushani hizo zikiendelea, baadhi ya wananchi walianza kurusha mawe, hali iliyowalazimu viongozi kufunga mkutano huku Jeshi la Polisi likiamuru wananchi kutawanyika.

0 comments:

Post a Comment