Tuzo zimezidi kumiminika katika klabu ya Chelsea baada ya
kocha wa timu hiyo Jose Mourinho
kutangazwa kuwa kocha bora wa msimu wa Ligi Kuu ya soka nchini England.
Tuzo hiyo inaifuatia ile aliyotwaa mchezaji Eden Hazard
ya kuwa mchezaji bora wa Ligi kuu ya soka nchini England msimu huu.
Jose Mourinho anatwaa tuzo hiyo baada ya kuiwezesha klabu
hiyo ya darajani kuwa mabingwa wa Ligi Kuu ya soka nchini England baada ya
kipindi cha takribani miaka mitano ya kutotwaa taji la Ligi Kuu.
Huu ni msimu wa pili kwa Mourinho kuifundisha klabu ya
Chelsea baada ya kutimkia katika vilabu vya Inter Milan na Real Madrid na msimu huu kurejea tena katika klabu ya
Chelsea.
Katika kinyang’anyiro hicho cha kocha bora wa msimu wa
Ligi ya England, Mourinho alikuwa akichuana na makocha wa timu nyingine kama
Ronald Koeman (Southampton), Arsene Wenger (Arsenal), Gary Monk wa Swansea City
na Nigel Pearson wa Leicester City.
Hii ni mara ya tatu kwa kocha Jose Mourinho kuchukua tuzo
ya kocha bora wa msimu kwani tayari alikwishachukua tuzo ya kocha bora wa msimu
katika misimu ya 2004-05 na 2006-07 akiwa na klabu ya Chelsea.
Msimu uliopita kocha wa Crystal Palace Tony Pulis ndiye
aliyekuwa kocha bora wa msimu baada ya kuiwezesha klabu hiyo kufanya vizuri na
kubaki Ligi kuu ya soka nchini England.
0 comments:
Post a Comment