Rais
wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi ameelezea hatua
zilizofikiwa katika utekelezaji wa Ilani yake siku 100 tangu alipoingia
madarakani.
Akizungumza
na waandishi wa habari leo (Februari 7 mwaka huu) katika mkutano uliofanyika
katika hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam, Rais Malinzi aliainisha
maeneo kadhaa yaliyopewa kipaumbele na tayari yameanza kufanyiwa kazi pamoja na
changamoto zilizopo.
Alisema
muundo wa Idara ya Ufundi umebadilishwa kwa kuundwa vitengo vya ufundi, elimu
na maendeleo ya mpira wa miguu huku maeneo ambayo tayari yameanza kufanyiwa
kazi kuwa ni;
Ujenzi
wa kituo cha mpira wa miguu (football centre of excellency), timu kupanda
daraja, kuanzisha mashindano mapya na kufufua ya zamani, mpira wa miguu wa
wanawake, maandalizi ya vijana (grassroot football), tiba, walimu na makocha,
utawala, uhusiano na Zanzibar, klabu za mpira wa miguu, wachezaji, masoko na
uwekezaji, kitengo cha habari, viwanja na timu ya Taifa (Taifa Stars).
Rais
Malinzi amesema changamoto zilizopo kwa sasa ni matumizi ya tiketi za
elektroniki, ufinyu wa bajeti, madeni, nidhamu, maadili na uchezeshaji wa
waamuzi.
Ametoa
mwito kwa wadau wote nchini wakiongozwa na Serikali, Shirikisho la Kimataifa la
Mpira wa Miguu (FIFA), Afrika (CAF), Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), vyombo
vya habari, mashirika ya umma na kampuni binafsi kushikamana na kuwa kitu
kimoja kwa nia ya kuinua kiwango cha mpira wa miguu Tanzania. (TAARIFA NZIMA YA
RAIS IMEAMBATANISHWA)
KILA LA KHERI
YANGA, AZAM
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linazitakia kila la kheri klabu za Yanga na
Azam ambazo timu zake zinatuwakilisha kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa
Afrika (CL) na Kombe la Shirikisho (CC).
Yanga
inacheza na Komorozine ya Comoro katika mechi ya kwanza ya raundi ya awali ya
CL itakayochezwa kesho (Februari 8 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
kuanzia saa 10 kamili jioni.
Nayo
Azam inaikaribisha Ferroviario de Beira ya Msumbiji katika mchezo wa kwanza wa
raundi ya awali ya CC utakaochezwa Jumapili (Februari 9 mwaka huu) saa 10
kamili kwenye Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi, Dar es Salaam.
Ni
matumaini yetu kuwa timu hizo mbili zitatuwakilisha vizuri kwenye michuano hiyo,
na kuwataka Watanzania wajitokeze kwa wingi viwanjani kuziunga mkono hasa kwa
vile zinacheza nyumbani.
TWIGA STARS
YAHAMISHIA KAMBI DAR
Timu
ya Taifa ya mpira wa miguu ya wanawake (Twiga Stars) imehamishia kambi yake
jijini Dar es Salaam kutoka Mlandizi mkoani Pwani ikiwa ni sehemu ya maandalizi
ya mechi ya michuano ya Afrika (AWC) dhidi ya Zambia.
Kikosi
hicho chini ya Kocha Rogasian Kaijage kimepiga kambi katika hosteli ya Msimbazi
Center kikiwa na wachezaji 25 kutoka 30 ambao kilianza nao katika kambi ya
Mlandizi mkoani Pwani.
Mechi
hiyo ya kwanza ya raundi ya kwanza dhidi ya Zambia itachezwa Februari 14 kwenye
Uwanja wa Nkoloma jijini Lusaka. Timu zitarudiana wiki mbili baadaye jijini Dar
es Salaam.
Wachezaji
waliopo katika kikosi hicho ni Amina Ally, Amisa Athuman, Anastasia Anthony, Asha
Rashid, Esther Chabruma, Eto Mlenzi, Evelyn Sekikubo, Fatuma Bashiri, Fatuma
Hassan, Fatuma Issa, Fatuma Mustafa na Fatuma Omari.
Wengine
ni Flora Kayanda, Happiness Hezron, Maimuna Said, Mwajuma Abdallah, Mwapewa
Mtumwa, Najiat Abbas, Pulkeria Charaji, Shelder Boniface, Sophia Mwasikili,
Therese Yona, Vumilia Maarifa, Winfrida Daniel na Zena Khamis.
PRISONS, RUVU
SHOOTING KUUMANA SOKOINE
Michuano
ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaendelea kesho
(Februari 8 mwaka huu) kwa mechi moja kati ya Tanzania Prisons na Ruvu Shooting
itakayofanyika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.
Mechi
nyingine nne za ligi hiyo zitachezwa keshokutwa (Februari 9 mwaka huu) kwenye
viwanja mbalimbali. Mgambo Shooting vs Simba (Mkwakwani, Tanga), Oljoro JKT vs
Kagera Sugar (Sheikh Kaluta Amri Abeid, Arusha), Rhino Rangers vs Coastal Union
(Ali Hassan Mwinyi, Tabora) na Mbeya City vs Mtibwa Sugar (Sokoine, Mbeya).
FDL YAANZA
VUMBI LA MZUNGUKO WA PILI
Mzunguko
wa pili wa Ligi Daraja la Kwanza (FDL) unaanza kesho (Februari 8 mwaka huu) kwa
mechi za kundi A na B wakati kundi C lenyewe litaanza mechi zake Februari 22
mwaka huu.
Mechi
za kundi A ni Green Warriors vs Tessema (Uwanja wa Mabatini, Mlandizi), Polisi
Dar es Salaam vs Transit Camp (Uwanja wa Karume, Dar es Salaam). Februari 9
mwaka huu ni African Lyon vs Villa Squad (Uwanja wa Mabatini, Mlandizi) na
Friends Rangers vs Ndanda (Uwanja wa Karume, Dar es Salaam).
Kundi
B kwa kesho (Februari 8 mwaka huu) ni Polisi Morogoro vs Burkina Faso (Jamhuri,
Morogoro), Lipuli vs Mkamba Rangers (Samora, Iringa), Kurugenzi vs Kimondo
(Wambi, Mufindi) na Mlale JKT vs Majimaji (Majimaji, Songea).
Boniface Wambura Mgoyo
Ofisa Habari na Mawasiliano
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)





0 comments:
Post a Comment