RUFANI KAMATI YA MAADILI MWISHO OKT 2
Wakati
walalamikiwa waliofikishwa kwenye Kamati ya Maadili ya Shirikisho la
Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) wakiwa wameshapokea uamuzi dhidi yao kwa
maandishi, mwisho wa kukata rufani Kamati ya Rufani ya Maadili ni kesho
(Oktoba 2 mwaka huu).
Walalamikiwa
wote saba waliohudhuriwa mashauli dhidi yao; Kamwanga Tambwe, Nazarius
Kilungeja, Omar Abdulkadir, Richard Rukambura, Riziki Majala, Shaffih
Dauda na Wilfred Kidao wamepokea uamuzi wa Kamati hiyo inayoongozwa na
Jessie Mnguto.
Kwa
mujibu wa Kanuni za Maadili, kwa ambao hawakuridhika na uamuzi huo
wanatakiwa kukata rufani Kamati ya Rufani ya Maadili inayoongozwa na
Jaji Mstaafu Stephen Ihema ndani ya siku tatu zinazomalizika kesho.
Rufani
ziwasilishwe kwa Katibu Mkuu wa TFF kabla ya saa 10 kamili jioni. Kwa
mujibu wa Kanuni ya 74 (1) na (2) ya Kanuni za Maadili, rufani
zikionesha sababu za kufanya hivyo zinatakiwa kuwasilishwa ndani ya siku
tatu kwa njia ya posta (registered post or dispatch or courier service)
kwa Sekretarieti.
Vilevile inatakiwa rufani inatakiwa kuambatanishwa risiti ya malipo ya ada ya rufani. Ada ya rufani ni sh. milioni moja.
MICHUANO YA CHALENJI KUANZA NOV 27
Michuano
ya Kombe la Chalenji inayoandaliwa na Baraza la Vyama vya Mpira wa
Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) inafanyika Kenya kuanzia Novemba
27 hadi Desemba 12 mwaka huu.
Nchi
wanachama ambazo zinataka kushiriki zinatakiwa kuthibitisha ushiriki
wao kwa Sekretarieti ya CECAFA kabla ya Oktoba 20 mwaka huu. Wanachama
wa CECAFA ni Burundi, Djibouti, Eritrea, Ethiopia, Kenya, Rwanda,
Somalia, Sudan, Sudan Kusini, Tanzania, Uganda na Zanzibar.
Michuano
hiyo itatanguliwa na Mkutano Mkuu wa CECAFA utakaofanyika Novemba 26
mwaka huu ambao pamoja na mambo mengine utakuwa na ajenda ya uchaguzi.
Uchaguzi huo ni kwa ajili ya kujaza nafasi nne za wajumbe wa Kamati ya
Utendaji.
Wajumbe
wanaomaliza muda wao ni Sahilu Gebremarian wa Ethiopia ambaye pia ni
Makamu Mwenyekiti wa CECAFA, Abdigaani Saed Arab (Somalia), Tariq Atta
(Sudan) na Raoul Gisanura (Rwanda).
Majina
ya wagombea yanatakiwa kuwa yamewasilishwa katika Sekretarieti ya
CECAFA kabla ya Oktoba 20 mwaka huu, na yakiwa yamethibitishwa na vyama
vyao vya mpira wa miguu.
SUALA LA PAPIC, YANGA LASUBIRI UAMUZI WA FIFA
Shirikisho
la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) limewasilisha rasmi suala la
madai ya aliyekuwa Kocha wa Yanga, Kostadin Papic dhidi ya klabu hiyo
katika Kamati ya Hadhi ya Wachezaji.
FIFA
imesema imepeleka rasmi suala hilo katika kamati yake hiyo baada ya
kupokea vielelezo vya Papic anayedai kuidai Yanga dola 10,000 za
Marekani pamoja na vile vya Yanga inayodai kumlipa kocha huyo fedha zote
alizokuwa akiidai klabu hiyo.
Kwa
taratibu za FIFA, hivi sasa haitapokea vielelezo vingine kutoka pande
hizo mbili, na badala yake Kamati hiyo inayoongozwa na Theo Zwanziger
kutoka Ujerumani itafanya uamuzi na kuziarifu pande husika. Zwanziger
kitaaluma ni mwanasheria.
Papic
aliyeinoa Yanga kwa vipindi viwili tofauti aliwasilisha malalamiko yake
FIFA akidai hadi mkataba wake unamalizika klabu hiyo ilikuwa haijamlipa
dola 10,000 za Marekani.
LIPULI, MAJIMAJI KUUMANA WAMBI FDL
Mechi
ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kati ya Lipuli ya Iringa na Majimaji ya
Songea sasa itachezwa kesho (Oktoba 2 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Wambi
uliopo Mafinga badala ya Uwanja wa Kumbukumbu ya Samora mjini Iringa.
Mabadiliko
hayo yamefanyika kutokana na Serikali kuutumia Uwanja wa Kumbukumbu ya
Samora kwa ajili ya shughuli za mbio za Mwenge.
Mechi
nyingine ya FDL kesho itakuwa kati ya Tessema FC ya Dar es Salaam na
Ndanda FC ya Mtwara, na itafanyika kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume
jijini Dar es Salaam.
Boniface Wambura Mgoyo
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
0 comments:
Post a Comment