Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan amezikosoa
vikali nchi za Afrika zinazotishia kujiondoa kwenye Mahakama ya
Kimataifa ya Jinai (ICC) akisema kuwa hiyo ni alama ya aibu na fedheha
kwa Afrika.
Annan aliyasema hayo katika sherehe ya kumuenzi Askofu Desmond Tutu
aliyekuwa miongoni mwa viongozi wa mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi
nchini Afrika Kusini na mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel mwaka 1984.
Annan amesema kama Waafrika wangeweza kutendewa uadilifu katika nchi zao
kusingekuwepo haja ya kwenda kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Jinai.
Amesema katika bara la Afrika ambalo limeshuhudia migogoro
iliyosababisha umwagikaji wa damu, ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu
na hata mauaji ya kimbari inashangaza kusikia watu wanasema kwamba
kutafuta haki katika mahakama ya ICC kutakwamisha juhudi za kurejesha
amani.
Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) inakosolewa sana na Waafrika
kwamba inawalenga viongozi wa bara hilo pekee na kufumbua jicho jinai
zinazofanywa na viongozi wa nchi za Magharibi katika nchi mbalimbali
duniani.
na radio tehranswahili
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment