Na Frank Geofray-Jeshi la Polisi.
Jeshi la Polisi Nchini limewataka Wananchi kufunga kamera maalumu za kuwatambua wahalifu (CCTV) katika maeneo yenye mkusanyiko mkubwa wa watu kama vile kwenye maduka makubwa, benki na kwenye nyumba za ibada ili kuweza kuwatambua wahalifu kwa urahisi pindi uhalifu unapojitokeza katika maeneo hayo.
Hayo yamesemwa na Msemaji wa Jeshi la Polisi Nchini,Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Advera Senso wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mikakati mbalimbali iliyowekwa na Jeshi hilo katika kupambana na wahalifu na uhalifu unaojitokeza hapa nchini.
Alisema hivi sasa Jeshi la Polisi Nchini linaendelea na utaratibu wa kutoa elimu kwa wamiliki wa Maduka makubwa, Benki na nyumba za ibada kufunga kamera hizo maalumu ambazo hurahisisha kumtambua mhalifu na hatimaye kukamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
“Tunawashauri kufunga hizo kamera na kufanya ukaguzi wa watu na magari yanayoingia katika maeneo yao ili kuhakikisha hakuna mhalifu anayepata mwanya wa kutekeleza uhalifu katika maeneo hayo muhimu ambayo kwa kiasi kikubwa yanakuwa na mkusanyiko mkubwa wa watu na sisi kama Jeshi la Polisi tutatoa ushirikiano mara moja pindi tutakapopata taarifa”Alisema Advera.
Aidha alisema hivi sasa wanaendelea na mpango wa kuimarisha usalama kuanzia ngazi ya familia ambapo kila Tarafa itakuwa na Askari 15 kulingana na hali halisi katika kata hizo ambapo kwa ujumla kwa nchi nzima ni Askari takribani elfu nane.
Alisema majukumu ya Askari hao katika Tarafa ni kuhakikisha kuwa uhalifu unapungua hasa kwa kushirikiana na kamati za ulinzi na usalama katika maeneo husika pamoja na kutoa elimu ya Ulinzi shirikishi ambapo kupitia mpango huo taarifa zz wahalifu zitafika mapema na kufanyiwa kazi kabla uhalifu haujatokea.
Alibainisha kuwa mpango huo tayari umeshaanza kutekelezwa katika mikoa mbalimbali hapa nchini ambapo katika jiji la Dar es Salaam tayari umeshazinduliwa katika mikoa mitatu ya kipolisi ambayo ni Ilala, Temeke na Kinondoni.
0 comments:
Post a Comment