Siku za hivi karibuni, ongezeko la huduma za mawasiliano nchini limekuwa kwa kasi sana. Huduma za mawasiliano nchini katika kipindi kifupi zimekuwa sana na kuwafikia Watanzania wengi zaidi. Kutoka laini za simu za mkononi milioni tatu tu mwaka 2000 hadi kufikia laini 28,000,000.
Watanzania walio wengi hivi sasa wanafaidika kwa huduma za mawasiliano, yakiwemo mawasiliano ya simu za mikononi, utangazaji. Vile vile huduma za ziada kama kutuma na kupokea fedha kwa kutumia mitandao na simu za mkononi zimeongezeka maradufu. Wananchi wengi wanapata huduma za kibenki kwa kutumia simu zao, wanawasiliana kwa kutumia simu zao kupitia sauti, SMS na kadhalika.
Hali kadhalika kumekuwa na ongezeko la matumizi ya intaneti kwa watanzania walio wengi kutoka watumiaji laki tatu miaka mitatu iliyopita hadi watumiaji milioni 7.6 kwa takwimu za hivi karibuni. Wengi wa watumiaji wa intaneti matumizi yao ni katika kujifunza na kujielimisha pamoja na matumizi ya mitandao ya kijamii kama vile Facebook, Twitter, BBM, LinkedIn na blog mbalimbali zinazotoa habari mbalimbali zikiwemo za kimaendeleo, burudani pamoja na michezo.
Matumizi haya ya intaneti yamewanufaisha watanzaia walio wengi kwani ni fursa murua ya kujifunza kupitia mitandao hiyo ya kijamii kwa kupata habari mpya, kujifunza na kuelimishana kuhusu shughuli za maendeleo na kuleta amani miongoni mwa watanzania.
Hata hivyo pamoja na maendeleo haya, kumekuwepo na baadhi ya watu wachache wanaotumia mawasiliano ya simu, mitandao ya kijamii, redio, TV na mawasiliano mengine kwa lengo la kuvuruga amani, kuchocheo vurugu, kuchonganisha watu, kusababisha ugomvi, kuwaumiza wengine kwa mambo yasiyo na ukweli, kupotosha jamii na hata kuvuruga maendeleo kwa ujumla.
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imezindua kampeni ya kuelimisha umma kuhusu matumizi mazuri ya mawasiliano na inawatahadharisha wananchi kwamba kutumia mawasiliano vibaya kama ilivyoainishwa katika sheria ya Mawasiliano ya Kielectroniki na Posta (EPOCA) ya mwaka 2010 ni makosa. Katika kampeni hii, Mamlaka inakusudia kuwasihi wananchi kuhakikisha wanatumia mawasiliano vizuri ili kudumisha amani, mshikamano na upendo miongoni mwa watanzania.
Watumiaji wa simu za mkononi na wananchi wote wanashauriwa kuunga mkono juhudi zinazofanyika ili kufanikisha kampeni hii kwa ajili ya kudumisha na kuendeleza amani na usalama na kuharakisha maendeleo ya sekta ya Mawasiliano inaendelea kuchangia uchumi wa Taifa na kuiweka Tanzania katika mazingira mazuri zaidi kijamii, kiuchumi na kisiasa.
Tunawasihi wananchi na watumiaji wa huduma za mawasiliano kuwa wakipokea ujumbe wowote wa kueneza chuki, unaopelekea kuvuruga amani, uchochezi na kuvuruga amani, toa taarifa kwa vyombo husika, kisha futa ujumbe huo. Usiueneze kwa wengine kwani utakuwa sehemu ya uhalifu.
IMETOLEWA NA
Tanzania Communications Regulatory Authority (TCRA),
Mawasiliano Towers,
20 Sam Nujoma Road,
Dar es salaam
0 comments:
Post a Comment