Serikali ya Jubilee nchini Kenya leo inaadhimisha siku 100 ofisini huku ikikabiliwa na changamoto nyingi kama vile mgomo wa waalimu, ukosefu wa usalama na hitilafu za kisiasa.
Mgomo wa wiki nne wa walimu ambao ulimalizika jana Jumatano ulitishia kuvuruga masomo ya wanafunzi wanaojitayarisha kwa ajili ya mitihani ya kitaifa.
Changamoto nyingine kubwa inayoikabili serikali ya Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto ni hitilafu za kisiasa zilizoibuka baada ya uchaguzi mkuu wa Machi 4.
Aidha serikali ya Jubilee imekuwa na wakati mgumu katika kudhibiti magenge ya wahalifu na mapigano ya kikabila katika maeneo kama vile Bungoma, Mandera na Tana River.
Uchunguzi wa maoni uliofanywa hivi karibuni na shirika la Ipsos Synovate unaonyesha kuwa asilimia 51 ya Wakenya wana imani na Rais Kenyatta huku 48 wakisema wana imani na Ruto.
Katika utekeleza wa ahadi za kampeni, serikali ya Jubilee imeidhinisha mpango wa kompyuta aina ya laptop kwa ajili ya shule za msingi, imeondoa malipo ya hospitali kwa akina mama wanaojifungua na imetenga dola bilioni sita kwa ajili ya Mfuko wa Wanawake na Vijana.
Katika anga ya sera za kigeni serikali ya Kenyatta imeonyesha azma yake ya kuboresha uhusiano na nchi za Afrika na Asia huku uhusiano wa Nairobi na Washington ukionekana kuzorota.
Aidha Uhuru na Ruto bado wanakabiliwa na kesi katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC.
Hatahivyo Umoja wa Afrika hivi karibuni ulibainisha upinzani wake kwa kesi hizo na kuitaja mahakama hiyo kuwa ya kisiasa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)





0 comments:
Post a Comment