Naibu
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dr. Seif S. Rashid.(Kulia) akiongea
na waandishi wa Habari hawapo pichani katika mkutano wa kutoa taarifa
juu ya madhimisho ya siku ya Wachangia Damu Duniani inayotarajiwa.
Ndugu Wananchi,
Tarehe
14 Juni 2013, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kupitia Mpango
wa Taifa wa Damu Salama inaadhimisha siku ya wachangia damu duniani.
Kidunia maadhimisho haya yatafanyika Paris nchini Ufaransa.
Kitaifa Maadhimisho hayamwaka huu yatafanyika Musoma Mkoani Mara katika
kiwanja cha Mkendo siku ya Ijumaa tarehe 14,Juni 2013 kuanzia saa 3
asubuhi na Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Afya na Ustawi wa
Jamii Dr Hussein Mwinyi (MB)
Madhumuni ya
maadhimisho haya ni kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa
kuchangia damu kwa hiari mara kwa mara ,kuwatambua, kuwaenzi na
kuwashukuru walewote ambao wamekuwa wakichangia damu kwa hiari mara kwa
mara bila malipo yoyote.
Ndugu Wananchi,
Duniani
kote, maelfu ya watu huokolewa maisha na damu ya watu ambao hawajawahi
kukutana nao, watu ambao huchangia damu yao ili kuwasaidia wengine.
Lakini mamilioni bado hawawezi kupata huduma ya damu salama pindi
wanapohitaji. Siku ya leo inatoa fursa ya kipekee kuwashukuru wale watu
maalumu ambao huchangia damu ili kuokoa maisha ya wahitaji. Tunaweza pia
kuongeza uelewa juu ya umuhimu wa kuchangia damu kwa hiari ili
Watanzania wajenge utamaduni wa kuchangia damu kwa hiari mara kwa mara
Ndugu Wananchi
Kauli
mbiu ya siku ya wachangia damu mwaka huu ni UCHANGIAJI DAMU NI ZAWADI
YA MAISHA. Maadhimisho haya yanaenda sambamba na madhimisho ya miaka 10
ya siku ya wachangia damu duniani.
Zawadi
kubwa ya thamani ambayo sisi binadamu tunaweza kupeana ni kuchangiana
damu, zawadi ambayo inaweza kuokoa maisha na kutoa nguvu mpya ya maisha
kwa watu wengi wanaohitaji tiba hii.
Kila
mmoja wetu anaweza kutoa zawadi ya maisha kwa kuchangia damu, ndiyo
maana dunia inaadhimisha siku hii ili kuwatambua watu ambao wamekuwa
wakitoa zawadi ya maisha kwa kuchangia damu kwa ajili ya kuokoa maisha
ya watu wengine
Ndugu Wananchi,
Kwanini uchangiaji damu ni zawadi ya maisha?
Damu
ni uhai na ina thamani kubwa, damu haipatikani viwandani wala
kuzalishwa sehemu yeyote ila kwa kuchangiwa na binadamu wenzetu.
Hivyo
zoezi la kuchangia damu ni endelevu na la kudumu, chupa moja ya damu
inaweza kuokoa maisha ya watu zaidi ya mmoja kama ikigawanywa kwenye
mazao ya damu kama vileplasma, chembe sahani na chembe nyekundu. Damu
inaweza kuhifadhiwa kwa muda wa siku 35 kabla ya muda wake wa kutumika
kwisha kulingana na virutubisho vilivyopo. Kutokana na uhifadhi wa damu
kwa muda mfupi ndiyo maana tunasisitiza umuhimu wa watu kuchangia mara
kwa mara. Kitaalamu mwanamume anaweza kuchangia mara nne kwa mwaka na
mwanamke mara tatu kwa mwaka.
Ndugu Wananchi,
Upatikanaji
wa damu kwa wakati huongeza nafasi ya kuishi kwa wahitaji wa damu,
huduma ya damu huokoa maisha ya mamilioni ya wagonjwa kila mwaka
duniani, Yafuatayo ni makundi makuu ya watu ambao huitaji damu:
•
Watoto
wadogo hasa walio chini ya umri wa miaka mitano kutokana na upungufu wa
damu unaosababishwa na malaria kali na magonjwa mengine (50%)
•
Wajawazito na wanawake wenye matatizo ya uzazi (30%)
•
Majeruhi wa ajali mbalimbali hasa ajali za barabarani na watu wanaofanyiwa tiba ya upasuaji (15%)
•
Wale
wote wenye magonjwa mbalimbali yanayosababisha upungufu wa
damu kamawagonjwa wa saratani, watu wanaosumbuliwa na seli mundu na
hemophilia (5%)
Ndugu Wananchi,
Tangu
kuanzishwa kwa Mpango wa Damu Salama Tanzania kumekuwepo na ongezeko la
wachangia damu wa hiari kutoka kiasi cha chupa 5,000 mwaka 2005 hadi
kiasi cha chupa 120,000 mwaka 2012. Hata hivyo kiasi hiki hakikidhi
mahitaji halisi nchini ambapo wastani wa chupa 400,000-450,000
zinahitajika kwa mwaka. Hii inaonyesha nakisi kubwa iliyoko ya
upatikanaji damu kwenye hospitali zetu. Nakisi hii mara nyingi imekuwa
inafidiwa na ndugu kuchangia damu ili kuokoa maisha ya mgonjwa. Lengo la
Mpango ni kukusanya damu kwa 100% toka kwa wachangiaji damu wa hiari.
Hata hivyo,
katika nchi nyingi Tanzania ikwemo, hakuna ugavi wa damu salama
unaotosheleza, na huduma za damu hukabiliwa na changamoto ya kupatikana
kwa damu ya kutosha, na wakati huo huo kuhakikisha ubora na usalama wa
damu hiyo
Usambazaji
wa damu ya kutosha unaweza kuwa wa uhakika kupitia uchangiaji damu wa
mara kwa mara na wa hiari usiohitaji malipo. Lengo la Shirika la Afya
Duniani (WHO) ni kwa nchi zote kupata mahitaji yao yote ya damu
inayohitajika kutoka kwa wachangiaji wa hiari wasiolipwa ifikapo mwaka
2020. Leo hii, ni nchi 62 tu, ambazo usambazaji wa damu kitaifa
unatokana na uchangiaji wa hiari usio na malipo takribani kwa asilimia
100, huku kukiwa na nchi 40 ambazo bado zinategemea wachangiaji wa
familia Tanzania ikiwemo.
Ndugu wananchi;
Katika
hatua ya kuboresha kazi za ukusanyaji, upimaji na usambazaji wa damu
hospitalini, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kupitia Mpango wa Taifa
wa Damu Salama umeanzisha mfumo wa kisasa wa tekinolojia ya habari
na Mawasiliano-ICT (Blood Establishment computer System) ambapo mpaka
sasa mfumo huu umeshafungwa katika kanda tano ambazo niKanda ya
Ziwa(Mwanza),Kanda ya Kaskazini(Moshi), Kanda ya Nyanda za Juu
Kusini(Mbeya), Kanda ya Mashariki (Dar-es-salaam) na Zanzibar
Katika
mfumo huu taarifa muhimu kuanzia kwa mchangiaji hadi damu inapomfikia
mgonjwa zitapatikana kwa urahisi. Vilevile mfumo huu utasaidia kutambua
wachangiaji wa mara kwa mara na hivyo kuweza kuongeza idadi ya
wachangiaji wa kudumu wa mara kwa mara(regular blood donors). Aidha
mfumo huu unasaidia kutambua viashiria mbalimbali ikiwemo kiasi cha
maambukizi ya magonjwa mbalimbali yanayosababishwa kwa kuongezewa damu
na hivyo kuhakikisha usalama wa mgonwa anayepewa damu. Pia mfumo
umerahisisha upatikanaji wa takwimu mbalimbali ikiwemo usambazaji wa
damu salama kwenye hosipitali zetu.
Pia katika
hatua za kuhakikisha Mpango unatoa huduma bora zinazoendana na viwango
vya kimataifa, Mpango umeanza mchakato wa kupata kibali (accreditation)
kwa ajili ya kanda za Mpango wa Damu Salama. Mchakato huu umeanza kwa
hatua ya kupitia miongozo na sera katika mtiririko mzima wa upatikanaji
wa damu salama na ukaguzi wa ndani. Katika hatua ya mwanzo inakadiriwa
ifikapo mwaka 2014 vituo viwili vya Damu Salama vitakuwa vimepata Cheti
kutambulisha kuwa vinatoa huduma kulingana na viwango vya kimataifa
Ndugu Wananchi,
Mpango
umeanzisha matumizi ya mitandao ya kijamii, hizi ni tovuti zilizoundwa
ili kuwezesha na kuongeza ufanisi wa mawasiliano baina ya mpango na
wadau wake. Lengo likiwa kuwafikia zaidi wananchi wote wa Tanzania
waliopo katika mitandao hii. Tovuti hizi ni kama “Facebook, Tweeter na
YouTube”. Uanzishaji wa mitandao hiiinaiwezesha Damu salama kujulikana,
kukuza na kuimarisha mahusiano mazuri kati ya damu salama na wachangia
damu, wafadhili na wadau wengine kupitia kubadilishana habari kwa njia
ya haraka na kwa wakati. Mpango unawasihi na kuwaomba wananchi kujiunga
kufuatilia na kutumia vyombo hivi ili kuongeza ufanisi waMpango wa
Taifa wa Damu Salama na hivyo kuongeza makusanyo ya damu toka kwa
wachangiaji wa hiari.
Ndugu Wananchi,
Nchini
Tanzania mahitaji ya damu yanazidi upatikanaji. Mpango wa Taifa wa Damu
Salama unakabiliwa na changamoto ya kuhakikishaupatikanaji wa damu
salama na ya kutosha ili kuweza kuwasaidia wagonjwa wanaohitaji damu
hospitalini. Mahitaji ya damu kitaifa ni wastani wa chupa
400,000-450,000. Mpango wa Taifa wa Damu Salama kwa sasa unakusanya
wastani wa chupa 120,000 kwa mwaka(26%). Hii inaonyesha nakisi kubwa
iliyoko ya upatikanaji damu kwenye hospitali zetu. Nakisi hii mara
nyingi imekuwa inafidiwa na ndugu kuchangia damu ili kuokoa maisha ya
mgonjwa. Lengo la Mpango ni kukusanya damu kwa 100% toka kwa wachangiaji
damu wa hiari.Mikakati kadhaa imewekwa kukabiliana na changamoto hii
kama tutakavyoona baadaye.
Changamoto nyingine ni kama ifuatavyo;
- Uelewa mdogo katika jamii kuhusu suala zima la uchangiaji damu kwa hiari kwani mfumo uliozoeleka ni ndugu wa mgonjwa kuchangia damu
- Uhamasishaji usiotosheleza toka kwa viongozi mbalimbali wa jamii,wanasiasa,viongozi wa dini nk.
- Uuzwaji wa damu usio halali hospitalini jambo mbalo linawakatisha tamaa wachangia damu wa hiari
- Matumizi yasiyo sahihi ya damu katika hospitali na
- Miudombinu hafifu hususan barabara duni wakati wa kukusanya na kusambaza damu
Ndugu Wananchi
Mpango wa Taifa wa Damu Salama umeweka mikakati ili kukabiliana na changamoto na kufikia malengo kama ifuatavyo;
- Kufanya kampeni ya kuhamasisha uchangiaji damu katika jamii (Community Campaign), Kampeni hii ina lengo la kuhakikisha upatikanaji wa damu ya kutosha wakati wanafunzi ambao ndio wadau wakubwa wapo likizo
- Kuongeza vituo vidogo vya kuchangia damu- “Blood collection satellite sites” katika sehemu mbalimbali za nchi. Kwa sasa Mpango una vituo vidogo vinne Dar-es-salaam- Mnazi Mmoja , Dodoma, Lindi na Morogoro ambavyo vina uwezo wa kukusanya chupa za damu 18,000 kwa mwaka
- Kushirikiana na uongozi wa mkoa kupitia mganga mkuu wa mkoa ili wilaya zitenge bajeti ya kukusanya damu kwa kushirikiana na Mpango wa Taifa wa damu salamaKufanya mkakati wa kujua matumizi halisi ya damu (Blood need assessment) nchini na kuendelea kuhamasisha madaktari, wauguzi na watumishi wa maabara juu ya matumizi sahihi ya damu
- Kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali Puplic Private Partnership(PPP) kuhakikisha Mpango unafikia malengo ya kukusanya chupa za kutosha za damu
- Kuendelea kuelimisha jamii kuhusu damu haiuzwi kwa kutumia vyombo vya habari na vipeperushi pia kutumia vifungashio vya damu (Blood bag) vyenye ujumbe “DAMU HAIUZWI”
- Kuendelea kuelimisha na kuhamasisha jamii (nje ya shule na vyuo) umuhimu wa kuchangia damu kwa hiari
- Kutoa majibu, na ushauri nasaha ndani yawiki mbili mpaka nne baada ya mtu kuchangia damu lengo ni kufikia 75% ya wachangiaji damu wa hiari ifikapo mwishoni mwa 2014. Kwa sasa Mpango umeweza kutoa majibu na ushauri nasaha kwa 58% ya wachangiaji damu wa hiari.
- Kuanzisha utaratibu wa kutuma ujumbe mfupi wa maandishi kwa njia ya simu kwa wachangia damu. Ujumbe huo utakuwa wa kuhamasisha, kumkumbusha mchangiaji siku ya kuchangia tena damu n.k
- Kuongeza utengenezaji wa mazao mbalimbali ya damu (Blood Products) toka30% ya sasa mpaka 50% mwaka 2014.
- Kuongeza kiwango cha asilimia ya wachangia damu wa mara kwa mara kutoka 20% kwa sasa (Repeat donors), hadi 50%ifikapo mwaka 2015 . Mpango utahakikisha unatembelea taasisi kwa ajili ya kuchangia damu angalau mara mbili kwa mwaka.
Ndugu Wananchi;
Uchangiaji
damu wa hiari wa bila malipo yoyote na wa mara kwa mara ni msingi wa
upatikanaji wa damu salama na ya kutosha. Wachangiaji damu wa kujirudia
ni salama kwani damu yao hainakiwango kikubwa cha maambukizo ya magonjwa
yanayoweza kuenezwa kwa njia ya damu. Lengo la Shirika la Afya Duniani
(WHO) ni kwa nchi zote kupata mahitaji yao yote ya damu inayohitajika
kutoka kwa wachangiaji wa hiari wasiolipwa ifikapo mwaka 2020
Ndugu Wananchi;
Natoa
rai/ujumbe kwa Watanzania kujenga utamaduni wa kuchangia damu kwa hiari
mara kwa mara ili nchi iwe na akiba ya damu ya kutosha , kwani asilimia
moja ya Watanzania wakiamua kuwa wachangiaji damu wa kujirudiaMpango
wa Taifa wa Damu Salama utaweza kukidhi mahitaji ya damu nchini.
NAMALIZIA
KWA KUSEMA NAOMBA WANANCHI WAJITOKEZE KWA WINGI SIKU HIYO ILI
TUONYESHE MSHIKAMANO NA KUTOA ZAWADI YA MAISHA KWA KUCHANGIA DAMU.
PAMOJA INAWEZEKANA
0 comments:
Post a Comment