Main Menu

Tuesday, April 16, 2013

LIGI KUU TANZANIA BARA (VPL) KUTIMUA VUMBI VIWANJA VITATU HAPO KESHO


Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaendelea kesho (Aprili 17 mwaka huu) kwenye viwanja vitatu huku vinara wa ligi hiyo Yanga wakifukuzia ubingwa huo jijini Tanga.

Yanga inayoongoza ligi ikiwa na pointi 52 itakuwa mgeni wa Mgambo Shooting katika mechi itakayochezeshwa na mwamuzi Athuman Lazi kutoka Morogoro kwenye Uwanja wa Mkwakwani. Waamuzi wasaidizi wa mechi hiyo ni Michael Mkongwa wa Iringa na Godfrey Kihwili wa Arusha wakati Kamishna wa mechi hiyo ni Godbless Kimaro kutoka Moshi.

Kagera Sugar na Toto Africans zitaumana kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba katika mechi namba 164 itakayokuwa chini ya mwamuzi Martin Saanya wa Morogoro.

Uwanja wa Manungu ulioko Turiani mkoani Morogoro, na wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 4,000 utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Mtibwa Sugar yenye pointi 33 na Oljoro JKT yenye pointi 28.

Israel Nkongo kutoka Dar es Salaam ndiye atakayechezesha mechi hiyo akisaidiwa na Hamis Chang’walu (Dar es Salaam) na John Kanyenye (Mbeya). Kamishna wa mechi hiyo ni Ramadhan Mahano kutoka Iringa.

AS FAR KUWASILI KESHO KUIKABILI AZAM
Wapinzani wa Azam katika michuano ya Kombe la Shirikisho, AS FAR Rabat ya Morocco wanatarajiwa kutua nchini kesho (Aprili 17 mwaka huu) saa 7 mchana kwa ndege ya Emirates.

Msafara wa timu hiyo wenye watu 28 utafikia hoteli ya Sapphire iliyoko maeneo ya Kariakoo, Dar es Salaam tayari kwa mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya pili itakayochezwa Jumamosi (Aprili 20 mwaka huu) saa 10 kamili jioni Uwanja wa Taifa.

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

0 comments:

Post a Comment