Mahakama ya juu zaidi nchini Kenya, imeamua kuwa rais
mteule Uhuru Kenyatta atasalia kuwa rais mpya wa Kenya baada ya kusema
kuwa uchaguzi ulifanywa kwa njia huru na ya haki.
Uamuzi huu una maana kuwa Uhuru Kenyatta ndiye ataapishwa kama rais mpya wa Kenya tarehe tisa mwezi ujao
Kesi hiyo iliwasilishwa katika mahakama ya juu zaidi na mpinzani mkuu wa Kenyatta, Raila Odinga baada ya uchaguzi uliofanyika mapema mwezi huu.
Matokeo rasmi yalionyesha kuwa Uhuru alishinda uchaguzi kwa kumpiku Raila kwa asilimia 50.07 huku Raila akipata asilimia 43.28. Matokeo haya yalizuia kufanyika kwa duuru ya pili ya uchaguzi kwa kura 8,100.
Bwana Odinga aliishutumu tume huru ya uchaguzi na mipaka kwa kuhujumu matokeo ya uchaguzi ili kumpa ushindi Uhuru Kenyatta.
Uchaguzi wa urais, wabunge na wajumbe wengine wa serikali, ulifanyika tarehe nne mwezi Machi, ukiwa wa kwanza tangu uchaguzi uliokumbwa na ghasia mwaka 2007 na kusababisha vifo vya watu zaidi ya elfu moja.
Bwana Kenyatta na mgombea mwenza wake ,William Ruto,wanakabiliwa na kesi katika mahakama ya jinai kwa kuchochea ghasia za mwaka 2007. Hata hivyo wamekanusha vikali mashtaka.
Mahakama ya juu zaidi inaweza kuthibitisha ushindi wa Kenyatta au kuubatilisha uamuzi wa wakenya na hivyo kuitisha uchaguzi mpya.
Vyovyote matokeo yatakavyokuwa kuna wale watakaoghadhabika mno.
Rais anayeondoka mamlakani, Mwai Kibaki amewataka wakenya kuwa watulivu na kukubali uamuzi wa mahakama lakini wengi wanatagemea sana idara ya mahakama ambayo imekuwa na mageuzi makubwa na ambayo sasa watu watu imani nayo.
Mawakili wa Odinga wanasema kuwa kesi yao ilihusisha madai ya kuhujumu hesabu ya kura pamoja na matatizo ya usajili wa wapiga kura na vile vile matatizo ya mitambo ya usajili wa wapiga kura.
Mnamo Ijumaa mahakama ya juu zaidi ilidurusu matokeo ya kura katika vituo 22 vya kupigia kura. Na pande zote mbili zilisema matokeo yalithibitisha misimamo yao.
Kenyatta ameutaja uchaguzi huo kama ishara ya kukuwa kwa demokrasia Kenya na ulifanywa kwa njia ya amani.
Tume ya uchaguzi, pia imesisitiza kuwa uchaguzi ulikuwa huru licha ya hitilafu za kimitambo
Wachunguzi wa kimataifa nao walisema kuwa uchaguzi ulikuwa huru na wa haki na kuwa tume huru ya uchaguzi uliendesha uchaguzi huo kwa uwazi.
chanzo bbcswahili.
0 comments:
Post a Comment