Timu ya Taifa ya
Tanzania (Taifa Stars), kesho jioni inatarajiwa kuondoka Addis Ababa Ethiopia
kuelekea nchini Misri tayari kwa mchezo wa siku ya jumapili.
Stars ambayo imeweka
kambi ya mazoezi takribani wiki moja sasa jijini Addis Ababa leo imeendelea na
ratiba yake ya mazoezi katika uwanja wa Taifa, ambapo leo imefanya mazoezi yake
asubuhi tu.
Kocha mkuu wa Taifa
Stars Mart Nooij amesema, maendeleo ya kambi ni mazuri timu yake inafanya
mazoezi katika viwanja viwili vizuri vilivyopo Addis Ababa, uwanja wa Taifa
na uwanja wa Benki ya Biashara ya Ethiopia.
Nooij amesema amekuwa akiwafundisha wachezaji
wake kucheza mpira wa kasi na pasi za haraka haraka, jambo ambalo wachezaji
wameonyesha kufuata vizuri maelekezo yake na kusema wanamuelewa vizuri.
Akiongelea mchezo
dhidi ya Misri siku ya jumapili, Nooij amesema timu inakwenda kupambana kusaka
matokeo mazuri katika mchezo, nafahamu tunaenda cheza ugenini, nimewaelekeza
vijana wangu wanaocheza nafasi ya ushambuliaji kutumia vizuri nafasi
tutakazozipata katika mchezo huo.
Aidha kocha Nooij
amesema katika mpira hakuna kinachoshindikana, kambi ya wiki moja Addis Ababa
imewasaidia wachezaji kukaa pamoja na kushika maelekezo yake vizuri, hivyo
anaamini timu yake itafanya vizuri katika mchezo huo wa kuwania kufuzu kwa
fainali za AFCON.
Katika kikosi cha
wachezaji wa 22 waliopo kambini jijini Addis Ababa hakuna mchezaji majeruhi,
wachezaji wote wako vizuri kiafya, kifikra na morali ni ya hali ya juu kuelekea
kwenye mchezo huo dhidi ya Mapharao.
Taifa Stars
inatarajia kuondoka kesho jioni ijumaa kuelekea nchini Misri kwa shirika la
ndege la Ethiopia majira ya saa 5 usiku na kufika Cairo majira ya saa 8 usiku,
kisha kuunganisha safari ya kuelekea jijini Alexandria ambapo timu mchezo huo
utakapofanyika.
Mchezo kati ya Misri
dhidi ya Tanzania utachezwa katika uwanja wa Borg El Arab kuanzia majira ya saa
1 jioni kwa saaa za huku, sawa na saa 2 kamili usiku kwa saa za Afrika
Mashariki.
Waamuzi wa mchezo huo
wanatokea nchini Ethiopia ambapo ni Bamlak Tessema Weyesa (mwamuzi wa kati),
Kinfe Yilma (mwamuzi msaidizi wa kwanza), na Wolday Hailerague (mwamuzi
msaidizi wa pili).
0 comments:
Post a Comment