Main Menu

Monday, January 14, 2013

WAGOMBEA TFF KUPATA FOMU KWENYE TOVUTI

Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) inawaarifu wadau wote kuwa fomu za maombi ya uongozi wa TFF na Tanzania Premier League Board (TPL Board) zinapatikana pia kwenye tovuti ya TFF.

Wote wanaopenda kugombea uongozi katika vyombo hivyo wanaarifiwa kuwa wanaweza kupata fomu hizo kwenye tovuti ya TFF (www.tff.or.tz) na wanatakiwa kulipia fomu hizo katika akaunti ya TFF namba 01J1019956700 iliyoko CRDB tawi la Holland House.



Fomu zikiambatanishwa na risiti ya malipo (receipt) au malipo ya benki (deposit slip) zirejeshwe kwa Katibu Mkuu wa TFF kwa mkono au kwa barua pepe (email) ambayo ni tfftz@yahoo.com kabla ya saa 10 kamili alasiri ya Januari 18 mwaka huu.


Kwa wagombea wanaorejesha fomu kwa mkono kuna fomu ya orodha (register) ambayo wanatakiwa kusaini wakati wanakabidhi.


Kamati ya Uchaguzi
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

PONGEZI KWA UONGOZI MPYA RUREFA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa pongezi kwa uongozi mpya wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Rukwa (RUREFA) uliochaguliwa katika uchaguzi uliofanyika Januari 10 mwaka huu.


Ushindi waliopata viongozi waliochaguliwa kuongoza chama hicho unaonesha jinsi wajumbe wa Mkutano Mkuu wa RUREFA walivyo na imani kubwa kwao katika kusimamia mchezo huo mkoani Rukwa.


TFF inaahidi kuendeleza ushirikiano wake kwa Kamati ya Utendaji ya RUREFA chini ya uenyekiti wa Blassy Kiondo aliyeibuka mshindi katika uchaguzi huo uliofanyika mjini Sumbawanga.


Uongozi huo mpya una changamoto nyingi, kubwa ikiwa ni kuhakikisha unaendesha shughuli za mpira wa miguu mkoani Rukwa kwa kuzingatia katiba ya RUREFA pamoja na vyombo vya mpira wa miguu vilivyo juu yake.


Pia tunatoa pongezi kwa Kamati ya Uchaguzi ya RUREFA na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa kuhakikisha uchaguzi huo unaendeshwa kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF.


Viongozi waliochaguliwa katika uchaguzi huo ni Blassy Kiondo (Mwenyekiti), Gregory Seko (Katibu), John Maholani (Mjumbe wa Mkutano Mkuu TFF), Ayoub Nyaulingo (Mwakilishi wa Klabu TFF) na Gloria Ndawa (Mweka Hazina). Nafasi nyingine zitajazwa katika uchaguzi mdogo.


HONGERA KWA AZAM KUTWAA KOMBE LA MAPINDUZI
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa pongezi kwa uongozi wa klabu ya Azam kwa timu yao kufanikiwa kutwaa Kombe la Mapinduzi mwaka huu.


Kwa Azam kufanikiwa kutetea ubingwa huo inaonesha jinsi klabu hiyo ilivyojipanga kabla ya kuingia katika mashindano hayo ambapo ilicheza fainali dhidi ya Tusker FC ya Kenya.


Pia ushindi huo utakuwa changamoto kwa timu nyingine za Tanzania Bara zitakazopata fursa ya kushiriki michuano hiyo ya Kombe la Mapinduzi mwakani. Michuano hiyo iko kwenye Kalenda ya Matukio ya TFF.


Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

0 comments:

Post a Comment