Main Menu

Thursday, April 4, 2013

VITISHO KATI YA KOREA KASKAZINI, KOREA KUSINI NA MAREKANI VYAENDELEA

Waziri wa Ulinzi wa Marekani Chuck Hagel

Serikali ya Korea Kaskazini imetangaza kuwa imeridhia uwezekano wa kufanya shambulizi la nyuklia. 

Marekani imesema inapeleka mtambo wa kisasa wa kuzuia makombora katika eneo la mpaka wa Marekani wa Guam, kama hatua ya tahadhari. 

Eneo hilo la Guam, lina idadi kubwa ya wanajeshi. 

Waziri wa Ulinzi wa Marekani Chuck Hagel amesema nchi hiyo haitayachukulia kama mzaha matamshi ya Korea Kaskazini, na hivyo itafanya kila iwezalo kujikinga dhidi ya mashambulio yoyote pamoja na washirika wake. 

Wakati huo huo, Korea Kaskazini leo kwa siku ya pili mfululizo imewazuia wafanyikazi kutoka nchi jirani ya Korea kusini kuingia katika kiwanda cha pamoja. 

Takribani magari 40 yalikuwa yakisubiri kuvuka mpaka kuingia katika kiwanda hicho cha Kaesong, lakini yakazuiwa kufuatia tangazo kuwa mpaka huo umefungwa. 

Jumla ya Wakorea Kusini 526 na magari 421 yalitarajiwa kuvuka mpaka huo leo kuingia Korea Kaskazini. 

Serikali ya Pyongyang iliiambia serikali ya Seoul kuwa imewazuia Wakorea Kusini dhidi ya kuingia katika kiwanda cha Kaesong ambacho kiko kilomita kumi ndani ya mpaka wa Korea ya Kaskazini.

0 comments:

Post a Comment