Main Menu

Wednesday, June 10, 2015

JACK WARNER AISHUTUMU MAREKANI KWA KUIKOMALIA FIFA



Aliyekuwa makamu wa rais wa shirikisho la Soka Duniani FIFA, Jack Warner, ameituhumu nchi ya Marekani kwamba inafuatilia mashtaka ya rushwa dhidi ya maafisa waandamizi wa shirikisho hilo kwa sababu imeshindwa kuwa mwenyeji wa kombe la dunia la mwaka 2022 zitakazofanyika nchini Qatar.

Tuhuma za Warner kuhusu Marekani ameziandika  katika gazeti Sunshine ambalo anamiliki huko Trinidad na Tobago,  Warner amesema tuhuma hizo dhidi yake na wengine kumi na tatu zinaonyesha kwamba Marekani inaegemea upande mmoja.

Warner amesema, Marekani inajifanya kuwa polisi wa dunia, imehamasika kuchukua hatua kuichunguza FIFA  baada ya kushindwa kuwa mwenyeji wa mashindano ya kombe la dunia ya mwaka 2022.

Warner, mwenye umri wa miaka 72 amekana tuhuma za kupokea rushwa ya dola milioni kumi za kimarekani kutoka Afrika Kusini baada ya kuchaguliwa kuwa mwenyeji wa michuano ya kombe la dunia ya mwaka 2010.

Katika makala yake, Warner ameendelea kujitetea kwa kusema kuwa, “kuishutumu Afrika Kusini kunachafua hadhi ya hayati Nelson Mandela ambaye ameisaidia Afrika Kusini kupata nafasi hiyo”.

Gazeti hilo limeonesha picha za Jack Warner akikutana na Prince William, David Beckham, Barack Obama na Vladimir Putin ambao amesema wote walikuwa na ushawishi pindi nchi zao zilipokuwa zikifanya kampeni ya kuwa mwenyeji wa Kombe la Dunia.

Jack Warner amemalizia kwa kuuliza iwapo walikuwa wanatumia takrima kama rushwa?

Jack Warner ni mmoja wa maofisa wa ngazi za juu wa bodi ya shirikisho la soka duniani FIFA, ambao wanatuhumiwa kwa kashfa ya rushwa na mpaka sasa Warner amekana tuhuma zote zinazomkabili.

0 comments:

Post a Comment