Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa
Stars) inatarajiwa kuingia kambini kesho jumatano katika hoteli ya Tansoma
iliyopo eneo la Gerezani jijini Dar es salaam kujiandaa na mchezo dhidi ya
Misri kuwania kufuzu kwa AFCON.
Kocha Mkuu wa Taifa Stars Mart Nooij,
amewaita wachezaji 16 kuingia kambini kesho siku ya jumatano kwa ajili ya
kupimwa afya zao na kujua maandeleo yao kabla ya kuwajumisha katika kikosi cha
pamoja kitakachokua kwenye maandalizi ya mchezo dhidi ya Misri.
Wachezaji walioitwa kuingia kambini kesho
ni, Mohamed Hussein, Peter Manyika, Hassan Isihaka, Jonas Mkude (Simba SC),
Salum Telela, Juma Abdul, Nadir Haroub (Yanga SC), Aishi Manula, Mudathir
Yahya, Frank Domayo, Kelvin Friday (Azam FC), Rashid Mandawa, Atupele Green
(Kagera Sugar), Haroun Chanongo (Stand United) Malimi Busungu (Mgambo JKT) na
Emmanuel Simwanda (African Lyon).
Mara baada ya kurejea kutoka nchini Afrika
Kusini, kocha wa Stars Nooij aliwapa mapumziko ya siku 10, wachezaji waliokua
kwenye michuano ya Cosafa mpaka Juni Mosi ambapo ndipo watajumuika na wachezaji
wengine waliopo kambini.
Ifikapo Juni Mosi, 2015 Taifa Stars itaanza
kambi ya moja kwa moja kujiandaa na mechi dhidi ya Misri itakayochezwa jijini
Alexandria katika uwanja wa Borg El Arab Juni 14, 2015 ikiwajumuisha pia
wachezaji Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wanaocheza soka la kulipwa katika
klabu ya TP Mazembe ya Congo DR.
Kabla ya kuelekea nchini Misri, Taifa Stars
inatarajiwa kuweka kambi jijini Addis Ababa nchini Ethiopia kuanzia tarehe
4,Juni 2015 kwa muda wa wiki moja kabla ya kuelekea nchini Misri kwenye mchezo
huo dhidi ya Mafarao.
Juni 20, 2015 Taifa Stars itawakaribisha
Uganda kwenye uwanja wa Aman mjini Zanzibar katika mchezo wa kuwania kufuzu kwa
Fainali za Afrika kwa wachezaji wa ndani CHAN, zitakazofanyika nchini Rwanda
2016, na mchezo wa marudiano kufanyika baada ya wiki mbili nchini Uganda.
0 comments:
Post a Comment