Taifa
Stars imemaliza vibaya mechi za mchujo za Kombe la Dunia, Kanda ya
Afrika baada ya kufungwa na Gambia huku Kocha Kim Poulsen akisema timu
yake imefungwa mabao mepesi.
Wenyeji
Gambia wameshinda mabao 2-0 katika mechi hiyo iliyochezwa leo (Septemba
7 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Independence ulioko hapa jijini Banjul
ukiwa ni ushindi wake wa kwanza katika kundi hilo la C ambapo imemaliza
ikiwa ya mwisho ikiwa na pointi nne.
Akizungumza
baada ya mechi hiyo, Kocha Poulsen amesema Gambia ilistahili kushinda
kwa vile ilitengeneza nafasi nyingi kuliko timu yake, na kuongeza kuwa
mabao iliyopata Gambia yalikuwa mepesi.
“Hatukutengeneza
nafasi nyingi za kufunga, lakini tukaruhusu mabao mapesi. Nawapongeza
Gambia kwani walistahili ushindi. Unapofanya makosa unaadhibiwa. Gambia
ilikuwa timu nzuri leo, kwani ilitengeneza nafasi nyingi za kufunga,
sisi tukatoa mabao mepesi,” amesema Kim.
Taifa
Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager imemaliza katika
nafasi ya tatu katika kundi hilo lililokuwa na timu nne ikiwa na pointi
sita ilizozipata nyumbani kwa kuzifunga Morocco na Gambia.
Hata
hivyo, Kim amesema sababu nyingine ya kutofanya vizuri ni kuwakosa
wachezaji wanaocheza nje ya nchi na wengine wa kikosi cha kwanza ambao
ni majeruhi.
Mabao
yote ya Gambia katika mechi hiyo iliyochezeshwa na Munyemana Hudu
kutoka Rwanda yalifungwa na nahodha wa timu hiyo Mustapha Jarjue.
Alifunga la kwanza dakika ya 44 na kupachika lingine dakika ya 51, mabao
yaliyotokana na wachezaji wa Stars kutokuwa makini.
Katika
mechi hiyo Stars iliwakilishwa na Juma Kaseja, Vincent Barnabas, Erasto
Nyoni/David Luhende, Nadir Haroub, Henry Joseph, Frank Domayo, Haruni
Chanongo, Amri Kiemba, Mrisho Ngasa, Simon Msuva na Khamis Mcha/Juma
Liuzio.
Taifa
Stars inaondoka Banjul kesho (Septemba 8 mwaka huu) saa 6 mchana kwa
ndege ya Arik hadi Dakar, Senegal ambapo itaunganisha kwa ndege ya Kenya
Airways kupitia Nairobi ambapo itawasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa
wa Julius Nyerere (JNIA) keshokutwa (Septemba 9 mwaka huu) saa 8.05
mchana.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
+2207362384 Banjul
0 comments:
Post a Comment