Main Menu

Thursday, September 5, 2013

KAMISHNA JENERALI WA MAGEREZA NCHINI AFUNGA MAFUNZO MAALUM YA KUTULIZA GHASIA MAGEREZANI, JIJINI DAR


Kamishna Jenerali wa Magereza Nchini, John Casmir Minja akitoa hotuba yake katika Ufungaji wa Mafunzo Maalum ya kutuliza Ghasia Magerezani leo Septemba 05, 2013 yaliyofanyika Kikosi Maalum cha Kutuliza Ghasia Magerezani.
Askari wa Kike pekee aliyemudu Kuhitimu Mafunzo Maalum ya kutuliza Ghasia Magerezani, Wdrs. Diana Nyaluta akionesha Ukakamavu wake pamoja na Ujasiri alionao alipoweza kuitumia kikwazo cha kamba kutambaa nayo huku akiwa amebeba silaha yake mgongoni aina ya Sub Machine gun(SMG) kama anavyoonekana.
Kamishna Jenerali wa Magereza Nchini, John Casmir Minja(wa kwanza kulia) akiangalia baadhi ya Vifaa ambavyo hutumiwa na Askari wa Kikosi Maalum cha Kutuliza Ghasia Magerezani wanapokuwa katika Operesheni mbalimbali za Kijeshi ikiwemo kutuliza Ghasia Magerezani zinapotokea (pembeni kushoto) ni Askari wa Kikosi Maalum akiwa amevalia Vifaa hivyo tayari kukabiliaa na ghasia yoyote.
Kamishna Jenerali wa Magereza Nchini, John Casmir Minja akimvisha kibaka cha rangi ya kijani Askari Wdr. Sostenes Mwacha kwa niaba ya Wahitimu wenzake kutokana na kufanya vizuri zaidi katika Mafunzo hayo Maalum ya Kutuliza Ghasia Magerezani leo Septemba 05, 2013 katika Kikosi Maalum cha Kutuliza Ghasia Magerezani, Ukonga Jijini Dar es Salaam.

Na Inspekta Lucas Mboje wa Jeshi la Magereza, Dar es Salaam

Kamishna Jenerali wa Magereza Nchini, John Casmir Minja amewaasa Askari wa Jeshi la Magereza nchini kuzingatia maadili ya kazi pamoja na kufanya kazi kwa bidii na kujituma wakati wote wanapokuwa wanatekeleza majukumu yao ya kila siku.

Kamanda Jenerali Minja ameyasema hayo leo wakati wa Ufungaji wa Mafunzo Maalum ya Kutuliza Ghasia Magerezani ya Kozi No.09 ya mwaka 2013 yaliyofanyika katika Kikosi Maalum cha kutuliza Ghasia Magerezani, Kilichopo Ukonga Jijini Dar es Salaam.

"Zingatieni maadili ya kazi pamoja na kufanya kazi kwa bidii na kujituma kwani ndiyo chachu ya mafanikio yoyote yale ya kazini au mafanikio yenu binafsi". Alisisitiza Kamanda Minja.

Aidha, akijibu hoja za changamoto mbalimbali zilizowasilishwa katika risala ya Wahitimu wa Mafunzo hayo Kamishna Jenerali wa Magereza Nchini, John Casmir Minja alisema kuwa tayari Ofisi yake imeanza kuchukua hatua ya kuzitafutia ufumbuzi changamoto hizo za upungufu wa vitendea kazi, makazi duni na upungufu wa Vyombo vya Usafiri kadri hali ya kifedha inavyoruhusu.

"Niwahakikishie kuwa kila jitihada zimekuwa zikifanyika na zitaendelea kufanyika kwa lengo la kuyatafutia ufumbuzi hatua kwa hatua matatizo haya kadri hali ya kifedha itakavyoruhusu". Alisema Kamanda Minja.

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo cha Kikosi Maalum cha Kutuliza Ghasia Magerezani, Kamishna Msaidizi wa Magereza, Rajabu Nyange amesema kuwa Mafunzo hayo Maalum ya Kutuliza Ghasia Magerezani yamechukua muda wa takribani miezi minane(08) na yalifunguliwa rasmi tangu Januari 04, 2013 ambapo Wahitimu hao wamejifunza mbinu za Medani za kivita, Magwaride ya aina mbalimbali, kutuliza Ghasia Magerezani, Upekuzi Maalum, Escort za aina mbalimbali.

Vile vile Wahitimu hao wamejifunza Haki za Binadamu, Sheria na Ustawi wa Jamii, Ukakamavu na Ujasiri, Utafutaji wa Wafungwa waliotorokea kwenye misitu minene, Utafutaji wa Mifugo pamoja na Matumizi ya Vifaa vya kuzuia moto.

Jumla ya Wahitimu 51 wa Kozi hiyo Maalum ya Kutuliza Ghasia Magerezani wamehitimu Mafunzo hayo ambapo kati yao Askari wa Kiume ni 50 na Askari wa kike 1 ambapo walijiunga na Mafunzo hayo mara tu baada ya kumaliza Mafunzo ya Awali ya Uaskari Magereza Kozi Na.26 Chuo Kiwira, Mbeya mwaka 2012.


0 comments:

Post a Comment