Main Menu

Friday, August 30, 2013

WIZARA YA MAENDELEO YA JAMII YALAANI MAUAJI YA MWANAFUNZI WILAYANI MAKAMBAKO NA UKATILI DHIDI YA MTOTO MKOANI RUKWA


Katika siku za hivi karibuni kumekuwepo na matukio mengi ya ukatili dhidi ya watoto ambayo yamekuwa yakiwaathiri watoto kimwili ikiwa ni pamoja na kupoteza maisha.

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa kuhusu tukio la mwanafunzi aliyepigwa na mwalimu wake katika shule moja ya Msingi Wilayani Makambako na kusababishiwa maumivu makali na hatimaye mtoto huyo akawa amepoteza maisha yake. Wizara inasikitishwa na mazingira ya kifo cha mtoto ambaye alikuwa chini ya uangalizi wa mwalimu na tukio la viboko ambavyo vinahusishwa na kifo cha mtoto.

Wizara inalaani vikali adhabu zinazotolewa kiholela kwa watoto bila kuzingatia kanuni na taratibu. Wizara inasisitiza kuzingatia utaratbu katika kuwarekebisha watoto ili adhabu ziwe na matokeo chanya kwa watoto na wanafunzi kwa ujumla. Kila mwanachi najukumu la ulinzi na usalama wa mtoto hivyo kwa pamoja tunatakiwa kushirikiana katika kuhakikisha kuwa familia na shule zetu zinakuwa mahala salama pa kuishi.

Katika tukio lingine, Wizara inakemea tukio la mama aliyemwunguza mtoto kwa moto katika sehemu za vidole vya mikononi kama sehemu ya adhabu kwa kosa la udokozi wa chakula. Wizara inasikitishwa na taarifa kuwa mtoto huyu amesababishiwa maumivu makali mwilini na inawezekana atapoteza kabisa vidole vya mkono mmoja katika maisha yake yote. Wizara inatoa rai kuwa adhabu kama hizi zinapotolewa na mmoja wa wanafamilia inarudisha nyuma jitihada za Serikali katika kukuza maendeleo ya haki za watoto nchini.

Aidha, kipigo cha mwanafunzi kilichosababisha kifo cha mwanafunzi na kumchoma mtoto mikononi ni matukio yanayochochewa na mitizamo finyu katika jamii katika kuwakanya watoto. Adhabu zenye madhara kwa mtoto hazimrekebishi mtoto na bala yake zinaleta madhara zaidi kwa maisha na uhai wa mtoto. Wizara inapenda kuwakumbusha wananchi kwamba Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasisitiza kuheshimu utu wa mtoto maana binadamu wote ni sawa na kwamba watoto nao wanastahili kupata haki sawa katika jamii.

Mwisho Wizara inaendelea kuhimiza jamii kubadilika na kuhakikisha kuwa shule na familia zinakuwa salama na mahali penye amani miongoni na wanafamilia bila kusahau kulinda na kuendeleza haki za watoto.

Wizara inatoa pole kwa wazazi, ndugu, marafiki na familia ya mwanafunzi aliyeuawa katika umri mdogo kutokana na kufanyiwa ukatili na Wizara inaomba jamii kuwa wavumilivu katika kipindi hiki kigumu.

Erasto T. Ching’oro
KNY KATIBU MKUU
30 Agosti, 2013


0 comments:

Post a Comment