Wakati Tanzania ikisema kuwa iko tayari kukaa meza moja na jirani yake Rwanda kumaliza hali ya uhasama iliyoanza kujitokeza katika siku za hivi karibuni, Katibu Mkuu wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dk Richard Sezibera amesema jitihada za kidipolomasia zinafanyika kutatua tofauti hizo za kimawazo.
Bila kutaja taasisi wala wanaohusika katika
jitihada hizo za kidiplomasia, Dk Sezibera aliwaambia waandishi wa
habari jijini Arusha jana kuwa jitihada hizo zinafanyika kimya kimya
bila kushirikisha vyombo vya habari “Migongano na tofauti za kimtazamo
miongoni mwa viongozi wakuu wa nchi wanachama wa EAC ni jambo lisilo la
afya kwa Jumuiya na linastahili kushughulikiwa kidiplomasia,” alisema Dk
Sezibera.
Akizungumza kwa tahadhari kubwa kukwepa kuingia
kwa undani kuhusu suala hilo, Katibu Mkuu huyo alisema inafaa kila
linalowezekana lifanyike kutatua mgongano wowote unaotokea kati ya
viongozi wakuu.
Mjini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe naye alisema katika mahojiano
kuwa iwapo Rwanda itaomba kukutana na Tanzania kwa ajili ya kumaliza
mzozo huo Serikali itakuwa tayari kutoa ushirikiano.
“Tanzania tunaona kuwa hii itakuwa njia ya busara
zaidi kumaliza tofauti zetu kwa njia ya mazungumzo badala ya kuendelea
kuishi kwa uhasama” alisema Membe na kwamba hali ya ujirani mwema na
tofauti zetu tuzimalize kwa njia ya mazungumzo.”
Waziri Membe alisema siyo jambo la busara kuacha
mzozo huo ukakaamuliwa na mataifa ya nje ili hali nchi zenyewe bado
zinafursa nzuri ya kukaa mezani na kujadiliana namna ya kutafutia
ufumbuzi mzozo huo.
Uhusiano wa Tanzania na Rwanda unatajwa kuwa
katika wakati mgumu kutokana na kauli za majibizano baina ya viongozi wa
pande zote mbili. Hivi karibuni Rais Jakaya Kikwete aliisihi Rwanda
kutotoa kauli za kejeli kwani kwa kufanya hivyo kunaweza kuhatarisha
uhusiano uliodumu kwa muda mrefu .
Hata hivyo, Dk Sezibera alisema tofauti na
migongano kati ya viongozi haiwezi kuathiri wala kuvunja Jumuiya ya sasa
ya Afrika Mashariki kama ilivyotokea kwenye Jumuiya ya awali mwaka 1977
kutokana utofauti wa muundo na misingi ya Jumuiya ya sasa.
“Jambo lililo dhahiri ni kwamba tofauti za
kimtazamo kati ya viongozi wa nchi wanachama (Kikwete na Kagame),
haziwezi kuhatarisha uhai wa Jumuiya ya Afrika Mashairiki kwa sababu
muungano huu umejengwa katika muundo na misingi imara tofauti na ule
(jumuiya) wa zamani,” alisema Dk Sezibera
NA gazeti mwananchi
NA gazeti mwananchi
0 comments:
Post a Comment