Main Menu

Thursday, August 1, 2013

BARAZA KUU LA USALAMA LAWATAKA WALINZI WA AMANI KUJIHAMI WANAPOSHAMBULIWA



Wakati watanzania wakiwa  bado hawajawasahau mashujaa wao Saba waliopoteza maisha wakati wakitekeleza jukumu la  ulinzi wa  Amani ya kimataifa katika jimbo la Darfur, nchini Sudan,   Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa, limetoa wito kwa walinzi wa Amani kudhibiti  mashambulizi yanayoelekezwa dhidi yao.


Wito huo wa Baraza Kuu la Usalama  umo ndani ya  Aya  zipatazo 30 za Azimio namba 2113 la mwaka 2013 ambalo limeongeza  muda wa   Mamlaka (   Mandate)  ya  Misheni ya Mseto ya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika inayolinda Amani katika  Jimbo la Darfur maarufu kama    UNAMID.


Katika kikao chake kilichofanyika siku ya  jumanne,  wajumbe 15 wanaounda  Baraza  Kuu la Usalama  walipitisha kwa kauli moja  Azimio hilo linaloongeza mamlaka ya UNAMID kwa  miezi 13 hadi  Agosti 31, 2014.


Miongoni mwa  Aya hizo 30 zipo aya zinazoelezea  kwamba ingawa kumekuwa na hali ya utulivu tangu  Misheni ya UNAMID ilipopelekwa   Darfur lakini pia  limeeleza kusikitishwa  kwake na uwepo wa matukio ambayo yanaelekea kudhoofisha hali ya amani na usalama na vile vile  kuvuruga shughuli za ulinzi wa amani na upelekaji wa misaada ya kibinadamu  kwa wananchi wanaokubwa na machafuko hayo.


 Baraza  Kuu kupitia Azimio hilo  pamoja na mambo mengine limelaani  vikali matukio ya kushambuliwa kwa  walinda Amani wa UNAMID,  likiwamo tukio la hivi karibuni    la Julai 13,  ambapo walinda amani   saba walipoteza maisha na wengine 14 akiwamo polisi kujeruhiwa katika shambulio la kushitukiza.


 Azimio hilo pia limesititiza   mamlaka ya    UNAMID ambayo  yapo  ndani ya  Sura ya    VII ya Katiba ya Umoja wa Mataifa, na kutoa wito kwa walinzi hao wa amani  kuzuia  vitisho vyovyote dhidi yao ikiwa  ni pamoja na kuwalinda wananchi  walio hatarini  bila kuathiri wajibuwa wa serikali wa kuwalinda  wananchi wake.  


Aidha  Baraza Kuu limesisitiza kupitia Azimio hilo   haja na umuhimu  kwa walinzi wa Amani  wa siyo tu kuwa tayari kukabili vitisho dhidi yao, bali limevitaka vyombo vinavyohusika kuhakikisha kuwa walinzi hao wanapewa zana na vifaa vitakavyowawezesha  kutekeleza mamlaka waliyopewa.


Vile vile kupitia Azimio hilo Baraza  limerejea tena wito wake wa kutaka uchunguzi wa kina ufanyike kuhusu tukio la Julai 13, na kwamba  ni matumaini yake kuwa  serikali ya Sudan itashiri kikamilifu kama ambavyo imekwisha kuahidi. 

Na aidha   Baraza limeyataka  makundi mengine kutoa ushirikiano   huku likisisitiza kwamba hujuma dhidi ya walinzi wa amani ni jambo ambalo halikubaliki Katika muktadha huo, na kupitia Azimio hilo, Baraza Kuu la usalama limezitaka pande  husika na  hasa  makundi  yenye    silaha na ambayo hayajatia saini  Nyaraka za   Doha kuhusu amani  ya Darfur , kuacha mara moja  vitendo vyovyote  vinavyolenga kuvuruga Amani na  kukomesha unyanyasaji na ukiukwaji wa haki za binadamu, mauaji holela.

Vile vile na  makundi hayo yametakiwa  kushiriki bila ya kuchelewa na bila masharti katika  mazungumzo ya kuteta Amani.



Aidha  Azimio hilo linamtaka  Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa kushirikiana na Umoja wa Afrika kuendelea  kupitia utekelezaji wa Mamlaka ya UNAMID  ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa kwa  Baraza hilo kila baada ya siku tisini.


Kupitia Azimio  hilo  Baraza  Kuu limezishukuru  nchi zote ambazo zimetoa wanajeshi wake na polisi kushiriki katika operesheni ya kulinda amani  kupitia UNAMID na limeyaomba  mataifa mengine kuendelea kuchangia kwa hali na mali ili hatimaye  UNAMID iweze kutekeleza majukumu yake kwa ukamilifu na kufanya Darfur kuwa mahali salama.



Wakati huo huo  akizungumza baada ya  Azimio hilo kupitishwa,   Muwakilishi wa  Jamhuri ya Sudan katika Umoja wa Mataifa, Bw. Daffa-Alla-Elhag Ali Osman, amelihakikishia Baraza  Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa, kwamba serikali yake itashiriki kikamilifu katika kuwasaka  wale wote waliohusika na tukio la  Julai 13.

na michuziblog

0 comments:

Post a Comment