Main Menu

Monday, March 11, 2013

WAMILIKI WA VYOMBO VYA HABARI VYA TELEVISHENI WATISHIA KUGOMA KAMA SERIKALI HAITAWASHA ANALOGIA

              Mkurugenzi wa makampuni ya Ipp Reginald Mengi

Baadhi ya Wamiliki wa vyombo vya habari vya televisheni nchini wamesema watafunga biashara ya kuonyesha matangazo iwapo serikali haitawasha mtambo wa analogia ili kwenda  sambamba na uliopo sasa wa digital.
 
Hali hiyo imefikiwa baada ya wamiliki hao kuona biashara yao inashuka na kukimbiwa na wateja wao kutokana na matangazo yao kuwafikia wananchi wachache tofauti na matarajio ya wadhamini wao kama ilivyokuwa kabla ya kuzimwa mtambo wa analogia.
 
Mwenyekiti wa wamiliki wa vyombo vya habari nchini Moat na Mmiliki wa kampuni ya IPP Reginald Mengi ameishauri serikali iwashe mtambo huo uwe sambamba na uliopo sasa wa digital ama watoe ruzuku ya ving’amuzi kwa wananchi ili kila mtu apate  haki yake ya kupata habari kama ilivyokuwa awali.
 
 
Nae Mkurugenzi wa kampuni ya Sahara Media  Samwel Nyara amesema serikali haikuwa na sababu ya kuharakisha kuzima analogia na kuwapa tabu wananchi wake ambao sasa wanakosa haki ya kupata matangazo kutokana na kushindwa kumudu gharama za ving’amuzi hivyo ameshauri uongezwe angalau mwaka mmoja kwa ajili ya maandalizi.

 
Tangu kuzimwa kwa mtambo wa analogia Desemba 31 mwaka jana, idadi ya watazamaji wa televisheni jijini Dar es salaam imeshuka kwa kiasi kikubwa kutokana na wananchi waliowengi kushindwa kumudu gharama za kununua ving’amuzi  hali inayosababisha wakose haki yao kikatiba ya kupata habari.
 

0 comments:

Post a Comment