Serikali ya Kenya ilionya hapo siku
ya Jumatano (tarehe 13 Machi) kwamba waandishi wote wa habari wa kigeni nchini
humo wasio na vibali maalum kutoka Wizara ya Habari na Mawasiliano
watashtakiwa.
"Tuna waandishi wengi wa kigeni
nchini mwetu na hatujuwi wanafanya kazi vipi," alisema Mkurugenzi wa
Mawasiliano Joseph Owiti, kwa mujibu wa kituo cha Capital FM cha Kenya.
"Tunaweza kuhitaji msaada wa maafisa wa usalama kuwatambua watu hao
waliopo hapa kinyume na sheria."
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Umma,
Mary Ombara, alisema serikali imekuwa na wasiwasi na "kazi mbaya
inayofanywa na baadhi wa waandishi wa kimataifa katika kuuripoti
uchaguzi."
"Katika hili, tunafurahi kwamba
vyombo vya habari vya hapa vilikataa kuchukua habari za uongo juu ya kununuliwa kwa maelfu ya mapanga au picha
iliyorushwa kuonesha ghasia ambazo hazipo nchini," alisema.
"Habari
lazima kila siku ziwe za ukweli na zisizopendelea upande wowote."
Mkuu wa Idara ya Leseni za Filamu,
Ernest Kerich, alisema waandishi wengi wa kigeni walioruhusiwa kuripoti
uchaguzi mkuu bado wapo nchini bila ya vibali muafaka.
"Tumejulishwa kwamba baadhi ya
waandishi wa habari waliendelea kubakia na kujihusisha na kutengeneza filamu
fupi wakitumia vibali vile vile walivyopewa," alisema Kerich.
"Hilo
sio tu linavunja sheria za nchi, bali pia linaikosesha nchi mapato."
0 comments:
Post a Comment