Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TFF Jamal Malinzi, ameitakia
kila la kheri timu ya Taifa ya Wanawake Tanzania (Twiga Stars) katika mchezo
wake wa kesho wa marudaino dhidi ya timu ya Taifa ya Zambia (She-Polopolo)
utakaochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Akiongea na wachezaji wa Twiga Star na benchi la Ufundi katika
chakula cha pamoja cha mchana leo katika hosteli za TFF zilizopo Karume, Rais
Malinzi amesema watanzania wote wana matumaini na timu yao kufanya vizuri
kwenye mchezo huo wa marudiano.
Aidha Rais Malinzi amewaambia bechi la ufundi na wachezaji wa
Twiga Stars kuwa pesa zote zitakazopatikana katika mchezo wa kesho baada ya
makato ya Uwanja na VAT, wagawane kwa pamoja wachezaji na viongozi.
Naye Mgeni mualikwa Ryhs Torrington ambaye ni Mkurugenzi wa kituo
cha Luninga cha Azam, alisema anaitakia kila la kheri Twiga Stars katika mchezo
wao wa kesho, na kusema mechi hiyo itaonyeshwa moja kwa moja na Azamtv, hivyo
waitumie vizuri nafasi hiyo kujitangaza kimataifa.
Kocha mkuu wa Twiga Stars Rogasian Kaijage na nahodha wake Sophia
Mwasikili, wamewahakikishia ushindi katika mchezo wa kesho, na kuwaomba watanzania kujitokeza kwa wingi
uwanjani kuja kuwashangilia.
Mechi inatarajiwa kuanza majira ya saa 10:30 jioni kwa saa za
Afrika Mashariki, na tiketi za mchezo zitauzwa kesho saa 2 asubuhi eneo la
Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, huku viingilio vya mchezo huo vikiwa ni
tsh. 5000 kwa VIP na tsh. 2000 kwa majukwaa yaliyobakia.
Twiga Stars ambayo katika mchezo wa awali iliibuka na ushindi wa
mabao 4-2, inahitaji sare ya aina yoyote ili kuweza kufuzu kwa fainali za
Michezo ya Afrika zitakazofanyika nchini Congo-Brazzavile mwezi Septemba.
0 comments:
Post a Comment