Ruvu Shooting imepigwa faini ya sh. 300,000 (laki tatu) kwa
kuzingatia Kanuni ya 14(9) ya Ligi Kuu kwa kutoingia kwenye vyumba vya
kubadilishia nguo (changing room) katika mechi namba 149 dhidi ya Kagera Sugar
iliyochezwa Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga
Pia Ruvu Shooting
imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa kutoingia vyumbani wakati wa
mapumziko kwenye mechi hiyo. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya
14(13) ya Ligi Kuu.
Stand United imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) baada
ya washabiki wake kuwatupia chupa za maji wachezaji wa akiba wa timu ya Polisi
Morogoro katika mechi iliyochezwa Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga. Adhabu
hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 42(1) ya Ligi Kuu.
Naye Meneja wa Polisi Morogoro, Manfred Luambano alitolewa
kwenye benchi la Polisi Morogoro kwa kosa la kutoa lugha za kashfa kwa mwamuzi
msaidizi namba moja Martin Mwalyanje. Suala lake linapelekwa kwenye Kamati ya
Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa ajili ya hatua za
kinidhamu.
Kipa wa Ndanda SC, Wilbert Mweta amefungiwa mechi tatu na
kupigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa kumkanyanga na kutaka kumpiga
mwamuzi Eric Onoka kwenye mechi namba 155 dhidi ya Polisi Morogoro iliyochezwa
Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro. Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya
37(5) ya Ligi Kuu. Kabla ya kufanya kitendo hicho alikuwa ameonyeshwa kadi
nyekundu.
Meneja wa Kagera Sugar, Mohamed Hussein anapelekwa kwenye
Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa kutoa lugha ya matusi kwa waamuzi na kutaka
kumpiga mwamuzi msaidizi namba 2, Said Mnonga kwenye mechi namba 158 dhidi ya
Azam FC iliyochezwa Uwanja wa Azam Compex jijini Dar es Salaam.
Naye Kipa Andrew Ntala wa Kagera Sugar amefungiwa mechi tatu
na kupigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa kuingia kwenye vyumba vya
waamuzi na kuwatolea lugha ya matusi mazito ya nguoni baada ya mechi hiyo.
Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 37(5)(c) ya Ligi Kuu.
Simba imepigwa faini ya sh. 300,000 (laki tatu) kwa
kuzingatia Kanuni ya 14(9) ya Ligi Kuu kwa kutoingia kwenye vyumba vya
kubadilishia nguo (changing room) katika mechi namba 159 dhidi ya Mbeya City
iliyochezwa Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya. Pia Simba imepigwa faini ya sh.
500,000 (laki tano) kwa kutoingia vyumbani wakati wa mapumziko kwenye mechi
hiyo. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(13) ya Ligi Kuu.
Mgambo Shooting imepigwa faini ya sh. 100,000 (laki moja)
kwa kuchelewa kufika kwenye kikao cha kitaalamu cha maandalizi ya mechi
(technical meeting) dhidi ya Ruvu Shooting. Mechi hiyo namba 161 ilichezwa
Uwanja wa Mabatini mkoani Pwani, na adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni
ya 14(2)(a) ya Ligi Kuu.
0 comments:
Post a Comment