Main Menu

Tuesday, September 17, 2013

LIGI KUU TANZANIA BARA YAINGIA RAUNDI YA NNE LEO

Michuano ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara imeingia raundi ya nne leo (Septemba 18 ) kwa mechi saba katika viwanja saba tofauti.

Vinara wa ligi hiyo, JKT Ruvu wanaonolewa na Kocha Mbwana Makata watakuwa ugenini Uwanja wa Mabatini ulioko Mlandizi mkoani Pwani dhidi ya Ruvu Shooting ya Charles Boniface Mkwasa. Mechi hiyo inatarajiwa kuwa kivutio kikubwa kwa washabiki mkoani Pwani kutokana na aina ya soka inayochezwa na timu hizo.

Baada ya sare dhidi ya Mbeya City wikiendi iliyopita, Yanga inaendelea kubaki Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya ambapo itacheza na Tanzania Prisons katika mechi itakayochezeshwa na mwamuzi Simon Mbelwa kutoka Pwani.

Nayo Simba itaumana na Mgambo Shooting Stars ya Tanga katika mechi itakayopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa viingilio vya sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000. Mechi hiyo itakuwa chini ya Kamishna David Lugenge kutoka Iringa.

Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Oljoro JKT kutoka Arusha na wenyeji Kagera Sugar wakati Azam na Ashanti United zitakwaruzana kwenye uga wa Azam Complex ulioko Chamazi jijini Dar es Salaam.

Mwamuzi Jacob Adongo kutoka Mara ndiye atakayechezesha mechi kati ya Coastal Union na Rhino Rangers itakayofanyika Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga. Mtibwa Sugar inarejea uwanja wake wa Manungu ulioko Turiani mkoani Morogoro ambapo inaikaribisha Mbeya City ya Kocha Juma Mwambusi.

Wakati huo huo, Ligi Daraja la Kwanza (FDL) nayo inaendelea leo (Septemba 18 mwaka huu) kwa mechi moja ambapo Lipuli ya Iringa ambayo wikiendi iliyopita ilicheza  na Mkamba mkoani Morogoro inapita mjini Morogoro kuikabili Polisi Morogoro kwenye Uwanja wa Jamhuri.


Boniface Wambura Mgoyo
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

0 comments:

Post a Comment