Kikao
cha Wajumbe wa Jukwaa la Wahariri kilichofanyika leo, Alhamisi, Oktoba 3, mwaka
2013, kimejadili uamuzi wa serikali kuyafungia magazeti ya Mwananchi na
Mtanzania.
Wajumbe
wa kikao hicho wamesikitishwa kwa hatua zilizochukuliwa na serikali dhidi ya magazeti
hayo. Baada ya mjadala wa kina, wajumbe wa Jukwaa wameazimia yafuatayo.
1.
Kupinga uamuzi wa serikali:
Jukwaa
linapinga hatua hiyo dhidi ya magazeti hayo kwa sababu adhabu hiyo imetolewa
kwa kutumia sheria kandamizi ya magazeti ya mwaka 1976 ambayo imekuwa
ikilalamikiwa na wadau kwa miaka mingi sasa.
Hii
ni moja ya sheria ambazo Tume ya Jaji Francis Nyalali ilipendekeza ifutwe kwa
sababu mbalimbali ikiwamo kukiuka misingi ya haki za binadamu, utawala bora na
kwenda kinyume cha Katiba ya nchi pamoja na maazimio ya kimataifa ya haki za
binadamu.
Hivyo,
tunaungana na taasisi nyingine kupinga adhabu hii kwa magazeti ya Mwananchi,
Mtanzania na wakati huo huo tukikumbushia kifungo cha gazeti la Mwanahalisi kwa
sababu sheria iliyotumika haifai.
2.
Tunalaani kufungiwa kwa magazeti:
Utaratibu
uliotumiwa na serikali kwa kujigeuza kuwa mlalamikaji, mwendesha mashitaka na
mtoa adhabu kamwe haukubaliki katika jamii yoyote iliyostaarabika kwa sababu ni
kinyume cha utaratibu wa kutoa haki
ya asili (natural justice). Hili si jambo la
kuendelea kufumbiwa macho na jamii ambayo inafuata misingi ya Kidemokrasia na
utawala bora.
Hivyo,
tunalaani kwa nguvu hatua hizi zilizochukuliwa kwa kukiuka misingi hii yote,
hasa ukizingatia kuwa ni serikali hii ambayo imesaini makubaliano ya kimataifa
kuhusu uwazi katika uendeshaji wa serikali (open government initiative).
3.
Nini kifanyike:
Tunafahamu
kuwa kuna kesi ya kuipinga sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 ambayo ilifunguliwa
mwaka 2009. Ni jambo la bahati mbaya na kusikitisha sana kuwa hadi hivi sasa,
miaka minne baadaye, bado kesi hiyo haijaanza kusikilizwa kwa sababu
haijapangiwa majaji.
Jukwaa
la Wahariri linapenda kutoa mwito kwa Mhimili wa Mahakama kurekebisha kasoro
hii kwa kupanga majaji kwa ajili ya kuisikiliza.
Kufanya
hivi kutahakikisha si tu haki kutendeka, bali pia haki kuonekana inatendeka.
Kuchelewesha haki ni sawa na kunyima haki.
Tunasikitika
zaidi kwamba serikali inaendelea kutumia sheria hii kandamizi huku ikiwa
imeikalia kwa miaka mingi sasa miswada ya sheria mbili muhimu zinazohusu haki
za habari bila ya kuziwasilisha bungeni. Kwa hiyo tunaitaka serikali
kuwasilisha miswada hiyo bungeni ili kupatikana kwa sheria mpya ya kusimamia
tasnia ya habari nchini.
4.
Hitimisho:
Hivyo
basi, tunatoa mwito kwa serikali kuyafungulia magazeti hayo.
Neville
Meena,
Katibu – Jukwaa la Wahariri
0 comments:
Post a Comment