Main Menu

Tuesday, December 24, 2013

MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI AWAKAANGA MAWAZIRI

  Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema amesema baadhi ya mawaziri wamekuwa wakaidi kufuata ushauri wa kisheria ambao amekuwa akiutoa na kwamba hicho ndicho chanzo cha matatizo yote yanayotokea katika utendaji wa Serikali, yakiwamo yale yaliyobainika katika Ripoti ya Operesheni Tokomeza Ujangili.


Wakati Jaji Werema akiwananga mawaziri, kwa upande mwingine amemsifia Rais Jakaya Kikwete akisema kuwa yeye si kama mawaziri wake kwani ni msikivu na anayeshaurika. Akizungumza na mwandishi wetu jana, Jaji Werema alisema endapo ushauri ambao amekuwa akiutoa mara kadhaa kwa mawaziri ungezingatiwa, kilichotokea bungeni mwishoni mwa wiki cha mawaziri kung’oka kisingekuwapo.

“Tunatakiwa kuiga msemo wa Mkuu wa Jeshi la Polisi, Said Mwema kuwa ‘tii sheria bila shuruti’, Rais tunamshauri na anashaurika kwa nini mawaziri wakatae kuzingatia ushauri?” alisema Werema na kuongeza:
“Mawaziri hawatakiwi kujifanyia tu mambo yao. Tunawaandikia barua lakini zinakwenda na yanafanyika yaleyale... Hata mimi nikionekana kukiuka sheria na kanuni naweza kuwajibishwa kwa kuwa hakuna aliye juu ya sheria.”

Jaji Werema alisema watu wanaweza kutofautiana kisiasa lakini katika mambo yanayohusu haki za binadamu lazima kuunganisha nguvu pamoja ili kuhakikisha sheria za nchi zinafuatwa bila kupindishwa.

Alikuwa akizungumzia kuhusu kung’oka kwa mawaziri wanne kutokana na matokeo ya uchunguzi wa Operesheni Tokomeza Ujangili ambao ulifanywa na Kamati ya Bunge ya Maliasili na Mazingira.

Ripoti ya Kamati hiyo ilisababisha Rais Kikwete kutengua uteuzi wa Mawaziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo David Mathayo na Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki.

Tume ya Kimahakama

Kadhalika, Jaji Werema alisema Tume ya Kimahakama itakayochunguza kwa kina madhara yaliyojitokeza katika Operesheni Tokomeza Ujangili iliyosababisha vifo, majeraha, utesaji wa kinyama, uharibifu wa mali na upotevu wa mifugo, itaundwa na Rais Kikwete.

“Tume hii itakwenda mbali zaidi ya taarifa ya kamati, itachunguza waliohusika, waliosemwa katika ripoti kwa juujuu watatafutwa, kuangalia matumizi ya nguvu kiasi hicho na mwisho mapendekezo ya tume hiyo juu ya kipi kifanyike kwa wahusika itazingatiwa,” alisema na kuongeza:

“Hawa Mawakili wa Serikali waliokuwa katika operesheni hiyo, DPP (Mkurugenzi wa Mashtaka) atatakiwa kutoa maelezo, hao mawakili wake walikwenda huko kwa misingi gani pamoja na mahakimu waliokuwa huko.”

Hata hivyo, Jaji mstaafu, Thomas Mihayo alisema hakuna haja ya kuundwa kwa tume hiyo na kinachotakiwa ni kutumika kwa sheria ya kutafiti sababu za vifo.


Alisema sheria hiyo ikitumika, wananchi watakwenda kutoa ushahidi mahakamani na wahusika kuchukuliwa hatua.

“Sijajua kwa nini sheria hii haitumiki hapa nchini, sisi tuliitumia mwaka 1972 baada ya kumtia hatiani aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi, Hamza Azizi kwa gari lake kusababisha kifo,” alisema na kuongeza:
“Nafikiri ataiunda mkuu wa nchi na ripoti kukabidhiwa kwake kwani waziri mkuu hawezi kukabidhiwa kutokana na kile kilichotokea bungeni kuwa ameshindwa kusimamia mawaziri wake.”

Kauli ya Jaji Mihayo iliungwa mkono na mtazamo wa Profesa Issa Shivji ambaye alisema watendaji, wakiwamo wa ngazi za juu, wafikishwe mbele ya mahakama kwa mashtaka ya kijinai.

“Mwanasheria Mkuu amependekeza uundaji wa tume ya kimahakama. Hii ni njia moja wapo lakini mara nyingi njia hii hutumika kama mbinu za kufunika kombe ili mwanaharamu apite,” alisema Profesa Shivji katika makala yake ambayo imechapishwa katika gazeti hili. Aliongeza: “Nionavyo, labda safari hii, Rais Kikwete anaweza kutumia njia mbadala ya kuteua mchunguzi huru ambaye atakusanya ushahidi na kuandaa mashtaka ya kupeleka mbele ya Mahakama.”

Alisema katika uchunguzi huo, watendaji wote wanaohusika, pamoja na wa kijeshi, usalama na wa kiraia, wachunguzwe na kushtakiwa bila kujali nyadhifa zao.

Msajili wa Vyama vya Siasa Mstaafu, John Tendwa alisema lengo la kuundwa kwa tume hiyo ni kuchunguza jambo fulani kwa kina ili kubaini chanzo na hatua za kuchukuliwa kwa wahusika huku ikiwa chini ya mwenyekiti ambaye ni jaji.

Tendwa alisema tume hiyo inaweza kushirikisha watu kutoka sehemu tofauti mbali na mahakama.
“Inakuwa chini ya jaji ili kuhakikisha haki inatendeka na si lazima wawe majaji watatu au wangapi lakini inajumuisha pia watu kutoka kada tofauti ndani ya mfumo wa kimahakama ili kuchunguza kwa undani tukio fulani,” alisema Tendwa.

CHANZO GAZETI MWANANCHI

0 comments:

Post a Comment