Mwomba rufani, Dr. Devota John Marwa, (Mrufani) ni msomi
mbobezi katika taaluma ya michezo, akiwa ni mhadhiri katika kitengo
kinachojihusisha na taaluma ya michezo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Akiamini kwamba anakidhi vigezo vilivyowekwa kwa nafasi ya mgombea uenyekiti wa
Chama cha Mpira wa Miguu wa Wanawake(TWFA), alichukua fomu ya kuomba kugombea
nafasi ya Mwenyekiti wa Chama hicho.
Maombi hayo yalikumbana na pingamizi zilizoletwa na wakereketwa
wawili wa soka la Wanawake, Bi. Chichi Mwidege na Bi. Mwajuma Noty, ambao kwa
pamoja walimwekea pingamizi Mrufani, kwamba hakidhi matakwa ya kanuni za
ugombea wa nafasi ya Mwenyekiti.
Waleta mapingamizi walidai kuwa Mrufani hakuwa na sifa
zilizoainishwa katika Kanuni za Uchaguzi za T.F.F. (TFF Electoral Code) Ibara
ya 9 (tisa) kipengele cha 3 (tatu), kinachomtaka mgombea awe amejihusisha na
uongozi wa mpira wa miguu kwa muda usiopungua miaka mitano.
Aidha Ibara ya 28 (ishirini na nane) kipengele cha 3
(tatu), kinamtaka mgombea awe amejihusisha japo miaka 2 (miwili) katika
shughuli za maendeleo ya mpira wa miguu nchini. Kamati ya Uchaguzi
iliridhia mapingamizi hayo na kuliondoa jina la Mrufani katika orodha ya wagombea
wa nafasi hiyo ya Mwenyekiti. Rufani hii ni matokeo ya uamuzi huo wa Kamati ya
Uchaguzi uliotolewa taraehe 22 Julai, 2015.
Kwa ujumla, sababu za kupinga maamuzi ya Kamati ya
Uchaguzi zinaweza kuhesabiwa kuwa ni mbili. Moja ni iliyojikita juu ya hitilafu
katika kuamua kwamba Mrufani hakuwa na uzoefu katika uongozi wa soka kwa muda
ulioainishwa. Sabau nyingine ni kwamba Kamati ya Uchaguzi illibua sababu ambayo
haikuwa katika Hati ya pingamizi iliyoletwa na Mleta pingamizi.
Wakati ambapo Mleta pingamizi alijikita katika
kipengele cha 28(3), Kamati iliibua kipengele cha 28(8), cha Katiba ya TWFA
kinachomtaka mgombea awe ametimiza uzoefu wa uongozi wa miaka mitano, ambacho
hakikuwemo katika hoja za pingamizi zilizowasilishwa na mleta pingamizi.
Katika kufikia uamuzi wake, Kamati ya Rufani ilizipitia
sababu za Mrufani kama zilivyoletwa, na baada ya kusikiliza maelezo ya Mrufani
na hoja za Mwakilishi wa TFF, Wakili Msomi Edward Augustino, na imeamua kama
ifuatavyo. Tutaanza na hoja ya mwisho.
Je, Kamati ilikuwa sahihi kuibua kipengele ambacho
hakikuletwa katika hati ya mapingamizi? Kamati inaweza kuibua kipengele hicho
endapo kwa kufanya hivyo, itakuwa imejielekeza katika nia njema ya maslahi ya
suala linalozungumziwa.
Sharti jingine ni kwamba hoja hiyo inyoibuliwa isiwe na
athari hasi(prejudicial) kwa mhusika. Kaika suala hili hata hivyo, hoja
iliyoletwa na Mleta pingamizi, yaani hoja chini ya kifungu cha 28 (3),
imeainisha kipindi kifupi cha uzoefu
(miaka 2), na hoja iliyoibuliwa na Kamati inahitaji
uzoefu wa miaka 5.
Endapo Mrufani angekuwa na uzoefu wa miaka 3 hadi 4, bado
angekwama kutokana na hoja iliyoibuliwa na Kamati. Hii kwa vyovyote ingekuwa ni
athari hasi (negative impact) katika harakati za Mrufani. Ni vema
Kamati zinazosikiliza malalamiko zikajikita kwenye
malalamiko yaliyoletwa na wahusika wenyewe. Kama pigamizi lingekuwa liko juu ya
kipengele hicho tu, tusingesita kukubaliana na sehemu hii ya rufani. Hata
hivyo, takwa la uzoefu wa miaka 5 limeainishwa pia katika Ibara ya 9 (3),
ambayo ilikuwa ni sehemu ya mapingamizi yaliyokuwepo kwenye hati ya mapingamizi.
Kwa sababu hiyo, Kamati ya Rufani haioni kama hoja hiyo
ina mashiko. Haitaitilia maanani. Hoja kuu ndani ya rufaa hii ni je, Kamati ya
Uchaguzi ilijielekeza vema kuhusu suala la uzoefu wa uongozi ulioainishwa na
Katiba?
Mrufani ameieleza Kamati ya Rufani mlolongo wa shughuli
ambazo amekuwa akizifanya, nyingi zikiwa zimejikita zaidi katika taaluma.
Miongoni mwa shughuli hizo ni kuandaa Mpango Mkakati wa kuendeleza soka la
wanawake. Mpango huu uliridhiwa na kuwasilishwa Makao Makuu ya Shirikisho la
Mpira Duniani, yaani FIFA.
Maelezo mengine ni kushiriki katika kuongoza timu mbali
mbali kule Chuo Kikuu, zingine zikiwa za watoto wadogo ambao baadhi ya matunda
yake ni wachezaji walioibukia kwake kama vile Simon Msuva. Alisema zaidi kuwa
alishiriki kuandaa warsha ilizoandaliwa kwa ushirikiano kati ya FIFA na TFF.
Aidha. Alisema kuwa amekuwa kiongozi tangu akiwa bado
kwenye vyuo vya ualimu, na baadaye alipohitimu na kufanya kazi kama Mwalimu,
kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam aliko mpaka sasa. Akasema,
hata alipokuwa Sweden kwa masomo ya juu pia lijihusisha na programu za
maendeleo ya soka la wanawake.
Wakili msomi wa TFF akijibu hoja hizo, alikubaliana na
uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi kuwa Mrufani hajaonesha popote kwamba amewahi
kuongoza soka, akasema Mrufani ni mtaalamu tu kama msomi, jambo linaloweza
kufanywa na msomi yoyote. Akamalizia kwa kuiomba Kamati ya Rufani za Uchaguzi
kuitupilia mbali rufaa ya Mrufani kwa kukosa mashiko.
Tofauti na Kamati ya Uchaguzi, Kamati ya Rufani imeona
kuwa kwa maslahi mapana ya mchezo wa soka katika ujumla wake, ni vema kuweka
tafsiri pana (wide interpretation) juu ya sifa zinazozungumzwa, badala ya kuweka
tafsiri finyu (restricted/narrow interpretation) kama ilivyofanya Kamati ya
Uchaguzi.
Baada ya kufanya hivyo, kuhusiana na Mrufani, Kamati
imeona kuwa ana sifa zinazostahili. Kupitia sababu alizozitoa, na vielelezo
vyake, Kamati ya Rufani haina wasiwasi kuwa Mrufani ana uzoefu mbali mbali sio
katika soka tu, bali pamoja na michezo katika ujumla wake.
Tumeshuhudia katika maelezo yake kwetu kwamba ushiriki
wake katika hatua mbali mbali, japo hakuwahi kuchaguliwa, sio ushiriki wa
kitaaluma tu, kama msomi mwingine yeyote. Ni ushiriki wenye dhamira ya dhati ya
kuleta mabadiliko/maendeleo katika soka la wanawake. Maelezo
yake kuwa aliaandaa programu ya maendeleo ya soka la
wanawake, hayakupingwa. Kamati ya Uchaguzi ingeangalia namna ambavyo “visheni”
iliyomo katika programu ile ambavyo ingeweza kutekelezwa na mtu aliyeaiandaa.
Kwa hiyo, katika hoja hii, Kamati inakubaliana kuwa Mrufani
anazo sifa stahiki, na kukatwa kwa sababu hii, Kamati ya
Uchaguzi haikujielekeza vema. Kwa hiyo, Mrufani ameshinda rufaa yake? Kamati ya
Rufani inachelea kujibu swali hili moja kwa moja. Utaratibu wa kuwasilisha
rufani ulikiukwa, na hapa ndipo rufaa hii inapokwaa kisiki. Chini ya
Ibara ya 13 (1) cha Kanuni ya
Uchaguzi (Electoral Code), mgombea ambaye hakuridhika na
maamuzi, atawasilisha rufaa yake ndani ya siku 3 (tatu) tangu uamuzi anaoupinga
ulipotolewa.
Kipengele cha 3 (tatu) cha ibara hiyo kinasema kwamba
Mrufani yoyote atakuwa na uhalali endapo rufaa yake imewasilishwa kwa mujibu wa
kanuni hizo. Uamuzi unaolalamikiwa ulitolewa tarehe 22 Julai 2015, sababu
za rufaa ziliandaliwa tarehe 27 Julai na sababu hizo za rufaa zililipiwa tarehe
28 Julai, 2015. Ni dhahiri kwamba rufaa ililetwa nje ya muda uliowekwa na
kanuni, na kwa hiyo inakosa uhalali kisheria na kikanuni.
Japo katika mwenedo na maamuzi yake Kamati ya Rufani za
Uchaguzi haifungwi na taratibu za kimahakama, suala la muda wa kuwasilisha
rufani sio miongoni mwa mambo ambayo Kamati inaweza kutoyazingatia. Kwa sababu
hiyo, Rufaa hii imetupwa, lakini kwa sababu tofauti na zile za Kamati ya
Uchaguzi.
Pamoja na uamuzi huu, Kamati ya Rufani za Uchaguzi
inapenda kwa namna ya kipekee kumpongeza Mrufani kwa jitihada alizozionesha
kutaka kuitumikia TWFA. Ni matumaini ya Kamati kuwa hatokata tama, na kwamba
atakuwa tayari, akitakiwa kufanya hivyo, kupitia taalum yake, kushirikiana na
wenzake katika jitihada za kuendeleza soka la akina mama lililo na changamoto
lukuki.
Imetolewa na,
JULIUS M. LUGAZIYA
Mwenyekiti-Kamati ya Rufani za Uchaguzi
0 comments:
Post a Comment