Main Menu

Monday, October 28, 2013

JAMAL MALINZI ACHUKUA MIKOBA YA TENGA TFF, AMBWAGA NYAMLANI KWA TOFAUTI YA KURA 12

RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) anayemaliza muda wake, Leodegar Tenga usiku wa kuamkia leo amemtangaza rasmi Jamal Malinzi kuwa rais mpya wa Shirikisho hilo baada ya kushinda uchaguzi wa rais wa TFF kwenye Ukumbi wa NSSF Waterfront, Dar es Salaam.


Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa, Malinzi alipata kura 73, huku mpinzani wake pekee Athuman Nyamlani akiambulia kura 52. Hii ni tofauti ya kura 21 kati ya mshindi Malinzi na Nyamlani.


Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, Hamidu Mbwezeleni ndiye aliyetangaza matokeo hayo na kuamsha shangwe ukumbini hapo huku wapambe wa wagombe wengine wakitoka vichwa chini.


Awali kabla ya uchaguzi huo, Nyamlani ndiye aliyekuwa Makamu wa rais wa TFF.


Kwa upande wa makamu wa rais wa TFF, aliyeshinda ni Wallace Karia aliyepata kura 67, akifuatiwa na Ramadhan Nasib aliyepata kura 52 na Iman Madega aliyepata kura 6 tu.


Kabla ya uchaguzi huo, Karia amewahi kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi inayoendesha Ligi Kuu ya Bara na Ligi Daraja la Kwanza.


KIDAU, MGOYI, KABURU, NYENZI WASHINDA UJUMBE

Katika uchaguzi wa wajumbe wa kamati ya utendaji, Wilfred Kidau alishinda kwa upande wa kanda ya Dar es Salaam akiwabwaga Alex Crispine Kamuzelya, Muhsin Said Balhabou na Omary Isack Abdulkadir. 

Aliyeshinda kanda ya Pwani na Morogoro ni Geofrey Nyange ‘Kaburu’ aliyewabwaga Farid Nahdi, Juma Abbas Pinto, Riziki Juma Majala na Twahil Twaha Njoki.

Khalid Mohamed ameshinda ujumbe kanda ya Tanga, Kilimanjaro akimshinda Davis Elisa Mosha. Naye Msafiri Mgoyi ameshinda kanda ya Tabora na Kigoma akimshinda Yusuf Hamis Kitumbo. 

Ayoub Nyenzi ameshinda kwa upande wa Iringa na Mbeya akiwashinda David Lugenge, John Exavery Kiteve, na Elias Mwanjala.

Kwa upande wa Ruvuma na Njombe aliyeshinda ni James Mhagama aliyemshinda Stanley William Lugenge. Naye Athuman Kambi ameshinda kanda ya Lindi na Mtwara akiwashinda Francis Kumba Ndulane na Zafarani Mzee Damoder. 

Na Blassy Kiondo ameshinda kanda ya Katavi, Rukwa akimbwaga Ayubu Nyaulingo.

0 comments:

Post a Comment