Vijana wengi wa kiume hujikuta
katika wakati mgumu kuchukua maamuzi ya kuishi na mwanamke japo yawezekana
wakawa wanatamani kufanya hivyo kwa muda mrefu kutokana na vikinza vingi,
vingine vikiwa ni vya kimaisha na vingine ni nadharia tu.
Katika bandiko hili, nitagusia sababu
kadhaa zinazochangia vijana wengi kujikuta wakisuasua au kuogopa kuingia kwenye
ndoa.
Kupanda kwa gharama za maisha
Kigezo hiki huwakumba zaidi wanaume
ambao wanaishi mijini. Gharama za maisha zimepanda sana kiasi kwamba mtu
anaweza kuwa anaishi peke yake na bado kuna mambo ambayo anashindwa
kuyatimiza kwa wakati, kama vile kozi ya nyumba, pesa ya kujikimu na mengine
mengi. Wengi huona ni heri kuwa na mtu tu ambaye ni mpenzi wake kuliko
kudhibiti kabisa kwa kuwa na huyo mtu kwa kuishi naye kwa hofu ya kushindwa
kutimiza wajibu. Ndio maana kwa wale ambao hupata akina dada ambao wanajiweza
kujitegemea na hivyo ni hodari kwa kusaidiana katika mambo ya kila siku hasa
katika masuala ya maendeleo huwa wepesi kuchukua maamuzi ya kuoa.
Utitiri wa wanawake wanaopatikana
kirahisi bila hata kuoa
Ni suala ambalo lipo wazi hasa
maeneo ya mijini akina dada/mama wa kuwa nao katika mahusiano (bila kujalisha
ni wa muda mfupi ama mrefu) wamekuwa wengi, rahisi kuwapata, wa kila aina
mwanaume watakao. Kuna wanaume wamejikita katika hilo kiasi kwamba mradi
tu atake mwanamke atatoka/atatumia namba alizohifadhi kwenye simu na
atafanikisha hiyo azima yake ndani ya siku hiyo hiyo ambayo amedhamiria bila
shida yoyote. Hii inafanya kwa kiasi kuchangia kwa wanaume kusuasua katika
maamuzi ya kuoa. Kwa kimombo hujiambia, “If I can get it for free, why buy it?”
Maradhi hasa ugonjwa wa UKIMWI
Pamoja na kuhamasishwa kwingi na
wataalamu wa maradhi ya HIV/AIDs kuwa mtu hata ukiwa umeathirika unaweza kuwa
na mahusiano na hata kuoa na kuwa na watoto; bado haisaidii sana kwa vijana
wanaojitambua kuwa ni waathirika wakiwa bado ni wadogo, hawajaoa/olewa ama
kuwahi kuwa na mtoto. Wengi sana hukata tamaa na huona ni kheri kubaki
walivyo kuliko kuingia katika ndoa. Naomba izingatiwe kuwa si wote; wengine
huwa hodari na huoa/olewa saa nyingine bila hata kumjulisha mpenzi wake huyo
kuwa yeye ana virusi chanya vya UKIMWI (HIV +ve).
Kufurahia ‘uhuru’
Hawa ni makapera wazoefu (wengine
husema ‘bachela sugu’), hakuna mtu ambaye anaweza mshawishi akabadilisha maisha
yake hayo ya kikapela (bachelor). Miaka huzidi kukatika hadi anafika miaka
takribani 40 au zaidi wala hana mpango wa kuoa na wala hajutii maamuzi yake
hayo. Mara nyingi wanaume wa namna hii hupenda sana wanawake (siyo lazima kuwa
atawachanganya kwa kuwa na zaidi ya mmoja); huwa na uwezo (hata kama
sustainable); Hutaka wanawake wadogo (mtu mzima sana kwake hapana hata kama
yeye ni mtu mzima); Ni mtu wa starehe sana, haoi kamwe na hufurahia uhuru huo
kwa hisia kuwa akioa ataupoteza uhuru wake.
Uhaba wa wanawake wanaofaa kuolewa
Na hii hutokea hasa kwa maeneo ya
mijini. Wadada/mama wengi wamekuwa ni ‘wa mjini’ mno, wajanja, malengo mbele
ikiwa imeambatana na tamaa, wanaoweka pesa mbele utu nyuma, wachanganyi (kuwa
na bwana zaidi ya mmoja). Haya mambo yamekuwa yakifanywa bila kificho,
inamfanya mwanaume anapokuwa katika mahusiano ahisi kuwa hata mtu wake ana
tabia hizo hizo hata kama siyo kweli. Hii inakatisha tamaa kwa wanaume wengi na
kuona wanawake wanaofaa kuoa (tokana na viwango vyake alivyoweka) ni adimu ama
hawapo kabisa!
Kutopata ampendaye kwa dhati
Kuna wanaume vigezo vya mwanamke awe
vipi havina umuhimu kabisa katika kutaka kuamua kuoa. Yeye kikubwa anataka
ampate mwamake ambaye atampenda kwa dhati na huku akiwa na matumaini kuwa huyo
mwanamke atampenda na yeye pia kwa dhati. Huyu mwanaume anaamini
msingi bora wa ndoa ni mapenzi ya dhati kati ya yeye na mkewe basi! Hana haraka
hadi pale atakapompata mwanamke akampenda. Kama huyo mwanamke atakubali kuolewa
ama lah; hilo ni suala jingine!
Mahusiano mabovu ya awali
Kuna wanaume huchagua wanawake kwa
sifa ambazo anazijua yeye mwenyewe. Yeye hamuangalii mwanamke kama mtu, bali
anamuangalia kama kitu. Daima vigezo vyake ni nataka mwanamke wa hivi, tabia za
vile, muonekano wa kule na mambo mengine kedekede. Hivyo unakuta kila siku yuko
katika mahusiano na mwanamke ambaye ni kweli anampenda kimuonekano; ila
linapokuja suala la tabia wanashindwana kabisa. Anaachana nae kisha anatafuta
mwingine kwa mtindo uleule – mwisho wa siku analaumu wanawake wote ni sawa na
kukata tamaa ya kuoa ama kusuasua katika maamuzi ya kutaka kuoa.
Kutoridhika na kipato chake
Kuna mwingine anaweza kuona
kutoridhika na kipato (ni sawa na sababu ya kwanza niliweka ya “Kupanda kwa
gharama za Maisha”) – lakini hii ni tofauti kidogo. Hapa namaanisha pale ambapo
mwanaume ana uwezo kabisa wa kuwa na mke na pia kuweza kukimu mahitaji yote
pamoja na ya familia yake. ILA kwa mipangilio yake anaona yeye bado; mara
nyingi wa hivi anataka ahakikishe ana uwezo wa kutosha ili aweze kuishi maisha
ya kifahari na si ya kujitosheleza tu. Hivyo katika hali ya kawaida ana uwezo
wa kuwa na mke lakini kwa maisha ya mtu wa kawaida na si wa kitajiri kama
malengo yake.
Malezi na Makuzi
Dhana mbovu juu ya ndoa
Dhana ya ndoa inaenda ikibadilika…
Kumekuwa na tabia ya watu kukatisha tamaa kwa kutoa vigezo, sababu, hadithi juu
ya ndoa ambazo ni za kubomoa kuliko kujenga. Sijui hawa watu hutumia vigezo
gani… HATA siku moja usitarajie uishi na mtu miaka nenda miaka rudi kitanda
kimoja, nyumba moja msigombane, kusiwe na madhaifu na pia kusiwe na wakati
ambao wote hadi kiwango cha kukata tamaa. Ndoa ni zaidi ya starehe na kufurahi…
Inahitaji nguvu kubwa, nguvu ya ziada, hekima, busara, kujituma na pia kuwa committed
kwa ndoa kuweza kufanikiwa. Sisemi kuwa lazima zote zitafanikiwa maana kuna
mambo ambayo yana mpaka – kuna wakati you just let go. Ila hakuna haja
ya kuibomoa hiyo taasisi kwa makusudi, taasisi ambayo ni msingi bora wa malezi
ya watoto kuliko taasisi yoyote ile inayoweza lea watoto ambao hasa ndiyo
tegemeo la vizazi vijavyo.
Kuzaa ovyo/Kuzaa kabla ya ndoa
Kuna wanaume wanazalisha balaa! Bila
kujalisha hizo mimba ni zao kweli ama wamesingiziwa kinachojalisha na watoto
hao kawakubali na anawalea. Kuna wanaume hadi anafikia umri wa miaka 30 tayari
ana watoto wa wanawake tofauti hata watano na analea. Kwa kiasi fulani, hii
inaweza mvunja morali ya kutaka kuoa, anaona kama watoto tayari anao na
anawalea hivyo hakuna haja ya kuwa na mwanamke kabisa ndani kama mke. Hii ni
mara chache.
Kukua kwa idadi ya wanawake
wanaotoka nje ya ndoa
Maadili mengi ya wanandoa yamezidi
kushuka… Hapo nyuma ilishazoeleka wanaume huwa na tabia ya kutoka nje ya ndoa
na wanawake kwa uchache. Bahati mbaya siku zinavyozidi kwenda idadi ya wanawake
wanaotoka nayo inakuwa kwa kasi, tabia ambayo inafanywa bila kificho kabisa na
imekuwa kana kwamba ni mashindano ya kutoka. Ni wazi thamani (reputation) ya
mwanamke ambaye anatoka na mwanaume anayetoka ni tofauti. Ni wanaume wachache
wana kifua cha kuweza kuvumilia mkewe/mpenziwe kutoka nje na kuendelea kuwa
naye. Kwa wanaume wengi ambao hawajaoa hili huchangia katika kukata tamaa ya
kupata mwanamke ambae anafaa kuwa mke na asiyeweza kuwa msaliti.
0 comments:
Post a Comment