Rais
wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga
amemshukuru Msajili wa Klabu na Vyama vya Michezo nchini kwa kusajili
Katiba ya TFF toleo la 2013 kutokana na marekebisho yaliyofanywa na
Mkutano Mkuu Maalumu uliofanyika Julai 13 mwaka huu.
Akizungumza
na Waandishi wa Habari, Dar es Salaam leo (Agosti 5 mwaka huu), Rais
Tenga ameishukuru Serikali, Msajili, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni
na Michezo, Dk. Fenella Mukangara, Naibu wake Amos Makala na Baraza la
Michezo la Taifa (BMT) kwa ushirikiano ambao wametoa kwa TFF katika
kufanikisha suala hilo.
Amesema
baada ya kupokea usajili huo, kinachofuata ni Katibu Mkuu wa TFF
kumwandikia rasmi Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ili aanzishe mchakato
wa uchaguzi wa viongozi wa TFF.
Kuhusu
kauli ya Naibu Waziri Makala kuwa marekebisho hayo yasingeweza
kusajiliwa kwa sababu hayakufuata Katiba ya TFF, Rais Tenga amesema
alikuwa ana haki ya kusema hivyo kwa sababu hakuwepo kwenye Mkutano huo,
na kuongeza:
“Makala
hakuwepo kwenye mkutano ndiyo maana alisema hivyo. Ana haki ya kuuliza,
nina hakika sasa atakuwa ameeleweshwa na ameelewa kwa sababu ni
msikivu. Kuhusu marekebisho hayo kupigiwa kura, hilo lisingewefanyika
kwa sababu hakukuwa na mjumbe aliyepinga marekebisho,” amesema.
Rais
Tenga amesema marekebisho hayo yalipitishwa kwa kauli moja (unanimous)
hivyo hakukuwa na sababu ya kuanza kunyoosha mikono kupiga kura, kwa
maana hiyo mkutano ulipitisha marekebisho kwa asilimia 100 wakati Katiba
ilikuwa ikihitaji theluthi mbili tu.
“Hakukuwa
na dispute (mabishano) kuhusu marekebisho, isipokuwa wajumbe walitumia
muda mwingi kuboresha kanuni na kutoa ushauri wa aina ya watu ambao
wangeingia kwenye kamati mbalimbali zikiwemo zile mpya za Maadili,”
amesema.
Ameongeza
kuwa kwa vile wote walioingia kwenye Mkutano Mkuu huo Maalumu ni watu
wa mpira wa miguu wasingeweza kupinga marekebisho kwa vile yametokana na
maagizo ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).
“Labda
itokee aliyeingia kwenye mkutano alikosea njia. Mtu yeyote wa mpira wa
miguu ni lazima afahamu kuwa maagizo ya FIFA ni lazima yatekelezwe, na
Katiba ya TFF inasema hivyo,” amesema Rais Tenga.
Pia
Rais Tenga amewataka wapenzi wa mpira wa miguu kushawishi watu wenye
sifa na uwezo wa kuongoza kujitokeza kwa wingi wakati Kamati ya Uchaguzi
itakapotangaza mchakato na tarehe ya uchaguzi huo.
AZAM YAANZA ZIARA KWA KUIKABILI KAISER CHIEFS
Makamu
bingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL), Azam wanaanza rasmi ziara ya mechi
za kirafiki nchini Afrika Kusini leo kwa kuikabili timu ya Kaiser
Chiefs ambayo inacheza Ligi Kuu ya nchi hiyo (PSL).
Kwa
mujibu wa Ofisa Habari wa Azam, Jaffer Idd aliyefutana na timu hiyo,
mechi hiyo inachezwa jijini Johannesburg. Idd anapatikana kwa namba +27788847399.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
0 comments:
Post a Comment