Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Wanawake Tanzania (TWB), Bi. Margareth Chacha akitoa elimu ya ujasiriamali kwa vikundi vya wanawake wajasiriamali katika mkutano uliofanyika jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.
Benki ya Wanawake Tanzania (TWB) imesema wateja wake ambao ni wajasiriamali wanawake kuanzia sasa watalipa marejesho ya mikopo yao kila mwezi ili kuwarahisishia shughuli zao kufanyika kwa mafanikio zaidi.
Awali, wateja hao ambao wako katika vikundi walitakiwa kulirejesha mikopo hiyo kwa kila wiki.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Bi. Margareth Chacha aliwambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki kuwa hatua hiyo imekuja baada ya kukubaliana na wateja wao ambao ni vikundi vya wajasirimali wanawake nchini.
“Marejesho ya mikopo yalikuwa yanafanyika kila wiki na wateja wetu…sasa tuna umri wa miaka minne na tunafahamiana vizuri,” alisema.
Alisema kuanzia sasa wanaotaka kulipa kwa mwezi wataweza kufanya hivyo na kwamba ni imani ya benki hiyo kuwa hatua hii itasaidia wajasiriamali hao kujiimarisha zaidi.
“Hatua hii itawasaidia sana wajasiriamali na jamii nzima kwa ujumla,” alisema,” na kuongeza kuwa mtu akitaka kuendelea ni sharti akope fedha kwenye mabenki.
Mkutano huo ulihudhuriwa na vikundi 69 na zaidi ya wanachama 600 ambapo walipaji bora wa mikopo na viongozi waliofanya vizuri walizawadiwa zawadi mbalimbali kwa kutambua mchango wao.
Aliwasisitiza wajasiriamali wanawake nchini wajiunge na vikundi mbalimbali ili waweze kupata mikopo kutoka benki yao na kufanyia shughuli za maendeleo.
Katika mkutano huo wanawake wengi walitoa ushuhuda kuwa tangu wajiunge na vikundi vyao na kupata mikopo wameweza kumiliki nyumba, magari na kusomesha watoto shule.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo ya Wanawake Mapambazuko, Bi. Salma Omari alisema kikundi chao kinafanya vizuri na wanachama wake wanarejesha kwa wakati mikopo.
“Tumeweza kujifunza mengi kutoka kwa viongozi wa benki hii ambayo imejitolea kutuwezesha,” alisema na kuongeza kuwa watahakikisha wanatumia fursa hiyo kujiendeleza kibiashara.
Alisema wanawake wanatakiwa kuamka na kujishughulisha kwa kufanya kazi mbalimbali zikiwemo za biashara kwa manufaa yao na familia badala ya kuwa tegemezi.
Kwa upende wake, mmoja wa wanakikundi cha Tabata 171, Bi. Zainabu Bwire alisema kikundi chao kina wanachama 40 na kinajivunia kuwa mteja wa benki hiyo kwa vile kinapata mikopo yenye riba nafuu.
Alisema wanawake wasikae tu majumbani kusubiri kuletewa na wanaume bali wajishughulishe kufanya kazi za kujipatia vipato.
0 comments:
Post a Comment