BAADA
ya sare mbili mfululizo, mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom
(VPL), Simba leo wanashuka Uwanja wa
Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya wakiwa wageni wa Tanzania Prisons.
Katika
mechi zake mbili zilizopita, Simba iliondoka pointi mbili tu kati ya
sita ilizokuwa ikizipigania. Ilitoka sare na timu za JKT Ruvu kwenye
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na baadaye sare ya 1-1 ugenini dhidi ya
Oljoro JKT.
Hiyo
itakuwa mechi ya nne kwa Mfaransa Patrick Liewig tangu aanze kuinoa
Simba huku akifanikiwa kuondoka na ushindi katika mechi moja dhidi ya
African Lyon inayokamata mkia kwenye ligi hiyo. Simba iliilaza Lyon
mabao 3-1.
Kwa
upande wa kocha Jumanne Chale anashusha kikosi chake uwanjani kesho
akiwa na kumbukumbu nzuri ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya
African Lyon katika mechi iliyochezwa kwenye uwanja huo huo Februari 9
mwaka huu.
Hekaheka
nyingine itakuwa Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza wenye uwezo wa
kuchukua watazamaji 25,000 utakapokuwa mwenyeji wa mechi kati ya Toto
Africans na African Lyon. Wakati Lyon ikikamata mkia, Toto Africans
yenye pointi 14 inashika nafasi ya 12 katika ligi hiyo inayoshirikisha
timu 14.
Uwanja wa sokoine jijini mbeya
Mwamuzi
Simon Mberwa wa Pwani atakuwa shuhuda wa mechi kati ya Coastal Union ya
Tanga na Oljoro JKT ya Arusha itakayofanyika Uwanja wa Mkwakwani jijini
Tanga. Mechi hiyo inatarajiwa kuwa na upinzani mkubwa kutokana na
uimara wa timu zote mbili.
Nayo
JKT Ruvu ambayo haijafanya vizuri msimu huu kulinganisha na minne
iliyopita itacheza Azam kwenye Uwanja wa Azam ulioko Chamazi, Dar es
Salaam. JKT Ruvu chini ya kocha Charles Kilinda inakamata nafasi ya nne
kutoka chini ikiwa na pointi 16 baada ya kucheza mechi 15.
Iwapo
itafanikiwa kushinda mechi hiyo, Azam itaendelea kujiimarisha katika
nafasi ya pili nyuma ya vinara Yanga. Azam ambayo ni moja ya timu zenye
safu kali ya ushambuliaji katika ligi hiyo ikiwa imefunga mabao 27 ina
pointi 33.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
0 comments:
Post a Comment