Main Menu

Wednesday, April 1, 2015

SIMBA WAINGIA MAKUBALIANO NA EAG GROUP KUONGEZA MAPATO



Ukitoa madhehebu ya dini na vyama vya siasa vilabu vya Simba na Yanga vinaweza kuwa vinafuata kwa kuwa na wafuasi wengi nchini.

Lakini nafasi ya wafuasi au mashabiki hao kuvisaidia vilabu hivyo bado imekua haionekani kutokana na sera ama mifumo ya vilabu hivyo kutokua na tija.

Unaweza ukashangaa kwa vilabu hivi ambavyo vina mashabiki kila uchochoro wa nchi hii kuwa na wanachama halali wenye kadi wanazozilipia wasiofikia hata elfu hamsini kwa kila klabu.

Kutokana na hali hiyo ambayo imeendelea kuzifanya timu hizo kuishi ndani ya ndimbwi la umasikini, klabu ya soka ya Simba imeingia makubaliano na kampuni ya EAG Group limited kwa lengo la kukuza mapato ya klabu hiyo.
Wakitiliana saini ya makubaliano ya miaka mitano (5) hii leo kwenye hotel ya Southern Sun, Rais wa klabu hiyo Evance Aveva amesema ili kujenga timu yenye ushindani ni lazima uwe na mfumo bora wa mapato na ndio maana mwezi uliopita walitoa zabuni ya kutafuta mshauri na mtekelezaji wa mkakati wa kuongeza mapata.

“kutokana na zabuni ile Simba Sports klabu imeridhishwa na wasifu wa kampuni ya EAG Group na hivyo basi kuipa kazi ya  kuwa washauri, watekelezaji wa mkakati wa kuanzisha na kukuza na kuendeleza mapato ya Simba” alisema aveva.

Ameongeza kuwa mikakati hiyo ikitekelezwa basi klabu hiyo itaweza kujenga uwanja wake, kupata mapato yatokanayo na jezi na vifaa vyenye nembo ya Simba, kuongeza wanachama naukusanyaji wa ada, kuanzisha zawadi kwa mchezaji bora wa timu, mchezaji mwenye nidhamu, na mchezaji bora kijana  mwenye kipaji.

“Mchezaji bora atapata gari, mchezaji kijana mwenye kipaji atapewa million tano na mchezaji mwenye nidhamu atapata million mbili pamoja na simu ya mkononi aina ya Huawei  ya kisasa kwa washindi wote” Alisema aveva.

Lakini pia klabu hiyo itaanzisha tuzo ya mchezaji aliyetukuka, Kuanzisha mfumo maalum wa taarifa kwa wanachama, Uanzishaji wa bidhaa mbalimbali na Kuongeza wadhamin.
 
Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa EAG Group Iman Kajula amesema lengo kuu la makubaliano hayo ambayo yataanza rasmi mwezi august ni kujenga mfumo wa ukuzaji mapato ya klabu hiyo kwa kuanzisha bidhaa na kuongeza wadhamin.

Amesema kupitia mkataba huo watahakikisha simba inakua moja ya timu inayovutia wachezaji hususani vijana kutaka kuichezea timu hiyo.

Jambo linguine ni utunzaji wa kumbukumbu za klabu wakati timu hiyo ikielekea kutimiza miaka themanini mwaka ujao na miaka mia moja badae.

Kuhusu uuzaji wa vifaa vya Simba, Kajula amesema lengo la makubaliano hayo si kuwazuia wauzaji wa sasa nafasi hiyo bali ni kutengeneza mfumo mzuri utakao nufaisha pande zote.

Katika mkutano huo na wanahabari rais aveva amegusia pia mazungumzo yanayoendelea na kampuni ya simu za mkononi ya Huawei ambayo imeanza kufanya kazi na klabu hiyo kwa washindi wa tuzo mbalimbali zilizotangwazwa ndani ya timu hiyo.

Suala la makubaliano ni kitu kingine na utekelezaji wake ni kitu kingine, kila la kheri klabu ya soka ya Simba katika makubaliano hayo ya miaka mitano.

0 comments:

Post a Comment