Siku chache baada ya kufungwa kwa pazia la udahili kwa wanafunzi
wa kidato cha sita walioomba kujiunga na vyuo vikuu nchini, imebainika
kuwa zaidi ya wanafunzi 5,000 wameshindwa kujiunga na vyuo hivyo
kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo matumizi ya mtandao wa kuomba
udahili.
Pazia la udahili huo kwa wanafunzi waliomaliza
kidato cha sita mwaka huu, lilifungwa rasmi Julai 5, mwaka huu. Hadi
wakati unafika tarehe hiyo, wanafunzi waliokuwa wameomba nafasi hiyo ni
39,140.
Matokeo ya kidato cha sita mwaka huu, yanaonyesha
kuwa watahiniwa 50,611 walifanya mtihani huo na kati yao 44,366 sawa na
watahiniwa wa shule waliofaulu ni 40,242 sawa na asilimia 93.92 ya
waliofanya mtihani huo.
Watahiniwa wa kujitegemea waliofanya mtihani huo
walikuwa ni 7,659 na waliofaulu ni 4,124 sawa na asilimia 53.87.
Kutokana na matokeo hayo, watahiniwa wote waliofaulu ni 44,366, hivyo
kufanya wanafunzi walioshindwa kujiunga na vyuo vikuu kuwa 5,226.
Akizungumza na Mwananchi Jumamosi, Mkurugenzi wa
Ithibati na Ubora wa Elimu ya Juu wa Tume ya Vyuo Vikuu Nchini (TCU), Dk
Savinus Maronga alisema, wanafunzi waliomaliza kidato cha sita na
kuomba kujiunga na vyuo vikuu ni 39,140 na kwamba vyuo vikuu nchini vina
uwezo kwa kuchukua wanafunzi 60,000.
Dk Maronga alisema hali hiyo inatokana na baadhi
yao kutokuwa na sifa zinazotakiwa kuweza kuomba udahili wa kumwezesha
kusoma elimu ya juu.
“Kuna baadhi hawana sifa ‘Eligibility’ za kuweza
kuchaguliwa kuingia Chuo Kikuu. Hivyo ili uweze kudahiliwa kuendelea na
elimu ya juu ni lazima uwe na vigezo. Kuhusu mfumo sidhani kama ulikuwa
na matatizo yeyote,” alisema Dk Maronga
Kauli za Wanafunzi
Wanafunzi waliozungumza na gazeti hili kuhusu
mfumo huo wa udahili wa mtandao, walisema una usumbufu kutokana na wengi
kutokujua kuutumia.
Frank Mabagala aliyehitimu Shule ya Sekondari Pugu
Jijini Dar es Salaam, alisema wanafunzi walio wengi wameshindwa
kuutumia mfumo huo kwani una mambo mengi ya kufanya.
“Nilijaza fomu vizuri tu, lakini sikuwa najua kama
kuna wakati nilitakiwa kwenda kuangalia ‘Eligibility’ hadi nilipoambiwa
na rafiki yangu kwenda kuangalia ‘Eligibility’ na kukuta kuna nafasi
imeandikwa ‘NO’ hapana vyuo vyote nilivyochagua,” alisema Mabagala.
Alisema hata upatikanaji wa vocha za TCU bado
zilikuwa tatizo, kutokana na kupatikana sehemu moja tu ya Benki ya NBC.
Hivyo kwa watu wanaoishi pembezoni mwa benki hiyo kuwawia vigumu kupata
huduma hiyo kwa haraka.
“Mfano mimi ninaishi Tegeta lakini nilikwenda benki pale Tegeta
nikakuta zimekwisha,.Nikaenda Mliman City nako nikakuta vivyo hivyo hadi
nilipokwenda Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ndipo nikazikuta nako
kulikuwa na foleni,” alisema Mabagala na kuongeza:
“Kama Dar es Salaam upatikanaji wa vocha inakuwa
hivi, je, kwa wanaoishi pembezoni mwa mkoa ambako benki kuifikia ni
kazi, watu wa aina hii watakuwa wamepata usumbufu mfano ni rafiki zangu
watatu wa mkoa walinitumia fedha huku ili niwanunulie vocha na
kuwatumia.”
Naye Zahora Miraji aliyehitimu kidato cha sita
Shule ya Seminari ya Ridwaa jijini humo, alisema alijaza fomu kulingana
na maelekezo yalivyokuwa, lakini katika hali ya kushangaza amekuta kile
alichokijaza kimebadilishwa.
Miraji alisema, katika chaguo la vyuo, chaguo la
kwanza na pili aliomba Chuo cha Mkwawa, la tatu na nne aliomba Chuo cha
Dodoma na chaguo lake la tano aliomba Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,
lakini alipokwenda kuangalia kwa mara ya mwisho akakuta amebadilishiwa.
“Nilijaza vizuri na nilipokuwa nikifungua kuona
kinachoendelea ninakuta bado iko katoka ‘mchakato’ lakini nilipokwenda
tena kuangalia nikakuta vyuo nilivyoomba vya Mkwawa, Dodoma na Dar es
Salaam vyote vimebadilishwa sasa sikujua tatizo ni nini,” alisema Miraji
na kuongeza:
“Nilikuta chagua la kwanza na la pili nimeandikiwa
chuo cha Jordan na hata sijui kipo wapi na chaguo la tatu hadi la tano
Chuo cha Usafirishaji Marrine. Nilikwenda TCU kuwaeleza kilichotokea
wakanipa fomu nikaijaza kuonyesha tatizo langu sasa sijui kama
watalishughulikia au la.”
Kauli ya Chuo
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,
Profesa Rwekeza Mukandala, alisema mfumo huu ni mzuri kutokana na
kuepusha usumbufu uliokuwepo awali.
Alisema kutokana na mabadiliko ya sayansi na
teknolojia ni lazima nchi ibadilike, kwa kuwa mfumo wa kujaza kwenye
makaratasi ilikuwa inaongeza ufanisi.
“Kama kuna matatizo hakuna budi kuufanyia
marekebisho ili uweze kutoa huduma kwa ufanisi lakini kweli ni mzuri na
siyo mwisho, kwani TCU wataufungua tena na wanafunzi wataweza kuomba
tena,” alisema Profesa Mukandala.
NA gazeti mwananchi.
NA gazeti mwananchi.
0 comments:
Post a Comment