Main Menu

Thursday, August 8, 2013

CCT YAPINGA UCHAGUZI KUFANYIKA SIKU YA JUMAPILI

Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) imewasilisha mapendekezo ya kuitaka Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala kubadilisha siku ya kupiga kura ya maoni ifanyike katika siku za kazi badala ya siku za ibada.

 
Akizungumza wakati wa kuwasilisha mapendekezo ya kuchambua muswada wa kura ya maoni katika kamati hiyo, Mwakilishi wa CCT, Mchungaji Lazaro Rohho alisema mabadiliko hayo yanatakiwa kuwekwa kwenye muswada wa kura ya maoni unaotarajiwa kuwasilishwa katika kikao kijacho cha Bunge.

 
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala William Ngeleja  

Alisema katika siku hizo za kazi, wananchi wanapaswa kupewa mapumziko ili waweze kufika kwenye vituo vya kupiga kura mapema, jambo ambalo linaweza kurahisisha kumaliza zoezi hilo mapema.

Alisema kutokana na hali hiyo, wanapaswa kubadilisha utaratibu huo ili watu waweze kushiriki kwa ufanisi katika ibada kwa sababu ni haki yao ya kimsingi.

Alisema, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec) inapaswa kuhakiki upya majina ya wapiga kura mwezi mmoja kabla pamoja na kusajili wapiga kura wapya ili wale wasiojiandikisha waweze kujiandikisha na wengine kuhakiki majina yao.

“Ikiwa wananchi watapewa elimu ya kutosha juu ya kura za maoni, wataweza kuona umuhimu wake na kujua haki za msingi ya kupiga kura, kutokana na hali hiyo, Serikali inapaswa kutumia zaidi ya mwezi mmoja ili kutoa elimu kwa wananchi juu ya suala hilo kabla ya kuingia kwenye zoezi la upigaji kura,” aliongeza.

Alisema hata hivyo, wafungwa wana haki ya kupiga kura, ila wamekosa uhuru, kutokana na hali hiyo muswada huo unapaswa kuongeza vipengele ambavyo vitaweza kuwatambua katika shughuli mbalimbali za upigaji kura na kimaendeleo.

Hata hivyo, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, William Ngeleja aliwataka wadau hao kuwasilisha mapendekezo yao kwa njia ya maandishi ifikapo Agosti 12 mwaka huu ili yaweze kufanyiwa kazi.

“Wale wote waliosema watawasilisha kwa maandishi wanapaswa kuleta Jumatatu kwa sababu ndio siku ya mwisho ya uwasilishaji wa mapendekezo hayo ili kamati iweze kuyapitia na kuyafanyia kazi kabla ya kikao kijacho cha bunge,” alisema Ngeleja.

Aliongeza, kutokana na hali hiyo, wadau walioitwa na kutoa maoni yao wanapaswa kuyapitia mapendekezo hayo ili waweze kuyafanyia kazi.

NA gazeti mwananchi

0 comments:

Post a Comment