HII NI HOTUBA YA ZITO KABWE BAADA YA KUSHINDWA KUHUDHURIA TAMASHA LA MATUMAINI JIJINI DAR
Leo
nilikuwa niwe nanyi kwa ajili ya siku hii muhimu sana kwa nchi yetu,
siku ya matumaini kama inavyoandaliwa na Kampuni ya Global Publishers.
Napenda kutoa shukrani zangu za dhati kabisa kwa ndugu yangu Erick
Shigongo kwa kuandaa tamasha hili kila mwaka. Nasikitika kuwa sitaweza
kufanya pambano la ngumi na ndugu Ray na pia kuchezea timu yangu ya
Wabunge wa Simba dhidi ya watani zetu Yanga. Hata hivyo naamini kuwa
tamasha litakuwa na mafanikio makubwa na nipo nanyi japo sipo Dar es
Salaam.
Ilikuwa niwepo Dar es Salaam leo, lakini nimeshindwa
kuondoka Marekani kwa sababu Spika wa Bunge Mama Anna Makinda ameniagiza
kwenye safari nyingine ndefu kwenda visiwa vya Cayman na baadaye
Namibia kwa shughuli za Umoja wa Wabunge wa Jumuiya ya Madola. Sikuweza
kukwepa jukumu hili la kitaifa maana limekuja ghafla na mimi nipo huku
jirani na maeneo hayo. Naomba radhi sana kwamba sipo nanyi leo.
Nawaomba muiombee amani nchi yetu na msimamie haki kwa wananchi wote
bila kubagua dini zao, rangi zao, hali yao kimaisha na ufuasi wa vyama
vya siasa. Mwaka huu tumeshuhudia matukio ambayo yanatikisa msingi wa
Taifa letu – Umoja. Hivi sasa msingi wetu una nyufa ambazo kwa kweli
hatujajua bado nini kinacholeteleza mambo haya kama kulipua makanisa,
kulipua mikutano ya vyama vya siasa na kuua viongozi wa dini.
Matukio haya yanatuelekeza kuwa makini sana na kauli zetu kwani baadala
ya kuunganisha wananchi tunawezajikuta tunawagawa zaidi Watanzania na
hivyo kuwa na mzunguko wa machafuko (vicious circle of violence). Ni
wajibu wa viongozi wa kisiasa na wananchi kuepuka kabisa kuanza
kurushiana maneno na lawama kuhusu matukio haya, kwani inawezekana
lawama na maneno yetu yakawa yanampa nguvu adui wetu ambayo hatujamjua
bado.
Napenda niwakumbushe kwamba ni rahisi sana kusambaza
chuki na ni vigumu sana kuondoa chuki miongoni mwa wananchi. Viongozi
hatari kama Hitler walitumia sana mbinu ya kueneza chuki dhidi ya jamii
ya Jews na matokeo yake yalikuwa ni vita vikuu vya pili vya dunia na
zaidi ya watu milioni 6 wasio na hatia kupoteza maisha. Sisi sote tuna
jukumu moja la kuhakikisha tunajenga Taifa lenye kujali HAKI na lenye
mshikamano mkubwa miongoni mwa raia. Kwa nia hii tu ndio tutaweza kuwa
na Taifa imara lenye heshima mbele ya mataifa mengine duniani. Ni kwa
njia hiyo tu ndio tutaweza kutokomeza umasikini uliokithiri mijini na
vijijini hapa nchini kwa kuongeza uzalishaji na kupanua ajira. Ikumbukwe
bila HAKI hakuna AMANI na bila UWAJIBIKAJI hakuna UTULIVU.
Tukiegemea siasa za CHUKI. Tukashindwa kuwa na mahusiano ya kawaida
miongoni mwa viongozi kuhusu masuala ya msingi ya nchi. Tukashindwa
kujadiliana kwa hoja kuhusu sera zetu. Tutapata viongozi aina ya Hitler
nchini mwetu. Wote tukatae. Sisi ni Watanzania. Muwe na Tamasha jema la
Matumaini.
Zitto Kabwe
7.7.2013, Aspen Colorado, USA.
0 comments:
Post a Comment