Mechi
za kwanza za hatua ya tatu ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) kuwania
nafasi tatu za kupanda Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu ujao zitachezwa
Jumamosi (Juni 15 mwaka huu) wakati za marudiano zitachezwa Jumatano ya
Juni 19 mwaka huu.
Kamati
ya Mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ilikutana
jana (Juni 11 mwaka huu) jijini Dar es Salaam kupitia ripoti za michezo
iliyopita na kufanya uamuzi mbalimbali ikiwemo mechi ya marudiano kati
ya Mpwapwa Stars na Machava FC ambayo haikuchezwa.
Machava
FC ambayo ilishinda mechi ya kwanza iliyochezwa mjini Moshi kwa mabao
2-0 inaendelea katika hatua ya tatu kwa vile haikuhusika katika
kukwamisha mchezo wa marudiano uliopangwa kuchezwa Uwanja wa Jamhuri
mjini Dodoma.
Chama
cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dodoma (DOREFA) kiliuhamishia mchezo huo
kwenye Uwanja wa Mgambo mjini Mpwapwa kinyume na maelekezo ya Kamati ya
Mashindano ya TFF. Kamati katika kikao chake cha awali iliekeleza kuwa
mechi zote za RCL zitachezwa makao makuu ya mikoa isipokuwa kwa Morogoro
ambapo timu ya Techfort FC iliruhusiwa kutumia Uwanja wa CCM Mkamba
mjini Ifakara.
Hivyo
timu nane zilizofuzu kucheza raundi hiyo ni Friends Rangers ya Dar es
Salaam, Kariakoo ya Lindi, Katavi Warriors ya Katavi, Kimondo SC ya
Mbeya, Machava ya Kilimanjaro, Njombe Mji ya Njombe, Polisi Jamii ya
Mara na Stand United FC ya Shinyanga.
Wakati
timu nyingine zimefuzu kwa kushinda mechi zao za raundi ya mbili,
Njombe Mji imeingia hatua hiyo kwa kuwa timu yenye uwiano mdogo wa
kufungwa (best looser) katika hatua ya pili.
Katika
hatua hiyo mechi ni ifuatavyo; Kariakoo vs Friends Rangers, Machava FC
vs Stand United FC, Polisi Jamii vs Katavi Warriors, na Kimondo SC vs
Njombe Mji. Timu zilizoanza kutajwa ndizo zinazoanzia nyumbani.
Vilevile
Kamati ya Mashindano imeagiza Kamishna wa mechi ya marudiano kati ya
Mpwapwa Stars vs Machava FC, Mwijage Rugakingira wa Tanga ambaye
alikwenda Uwanja wa Mgambo badala ya Uwanja wa Jamhuri kinyume na
maelekezo ya TFF aondolewe kwenye orodha ya makamishna.
Pia
waamuzi wa mechi hiyo ambao nao walikwenda Mpwapwa badala ya Dodoma
Mjini wamepelekwa Kamati ya Waamuzi ya TFF kwa ajili ya kuchukuliwa
hatua kutokana na tukio hilo.
Kamati
ya Mashindano imekumbusha kuwa RCL ni mashindano yanayosimamiwa na TFF,
hivyo maelekezo yoyote kuhusiana na mashindano hayo pia yatatoka TFF na
si mahali pengine popote. Hivyo, msimamizi wa kituoa hana mamlaka ya
kubadili uwanja.
Hatua
ya nne ya RCL itachezwa kati ya Juni 23 na 23 mwaka huu wakati mechi za
marudiano zitachezwa kati ya Juni 29 na 30 mwaka huu.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
0 comments:
Post a Comment