Main Menu

Monday, June 10, 2013

CHADEMA WAKUBALIANA NA RASIMU YA KATIBA

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema nchini Tanzania, ameweka wazi kuwa, chama chake kinaunga mkono Rasimu ya Katiba na hasa suala la Muungano wa Tanzania kuundwa na Serikali tatu kama ilivyopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya nchi hiyo.


Amesema mambo mengi yaliyopendekezwa na chama chake yamefanyiwa kazi na Tume ya Mabadiliko na kushangazwa  na CCM kwa kupinga rasimu hiyo hususan suala la serikali tatu wakati kimsingi watu wa Tanzania Bara wamekuwa wakipunjika kwenye muundo wa sasa wa muungano. 


Akihutubia mkutano wa kampeni ya kuwania udiwani wa Kata ya Iyela katika Uwanja wa Bongonela, Mbeya hapo jana, Mbowe alisema chama chake kinataka kuona Serikali ya Tanganyika ikifufuliwa tena. 


Alisema Chadema inataka kuona Wazanzibari wakiwa na serikali yao ili wajiamulie mambo yao wenyewe na pia Watanganyika wawe na uongozi wao lakini waunganishwe na serikali ya Muungano.


Aidha amesema kuwa, muundo wa sasa wa Muungano una matatizo, ambapo mbunge wa Zanzibar anawakilisha watu wachache zaidi akilinganishwa na  mbunge wa Bara, huku wote wakilipwa mshahara sawa.

0 comments:

Post a Comment