Main Menu

Tuesday, May 7, 2013

TAARIFA MBALIMBALI KUTOKA TFF MAY 07 2013

RED COAST, KARIAKOO, SAIGONI KUANZIA NYUMBANI RCL
Upangaji ratiba (draw) ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) umefanyika leo (Mei 7 mwaka huu) huku mabingwa wa mikoa ya Dar es Salaam (Red Coast), Lindi (Kariakoo) na Kigoma (Saigoni) wakianzia nyumbani katika ligi hiyo itakayoanza Mei 11 au 12 mwaka huu.

Ligi hiyo itachezwa kwa mtoano kwa mtindo wa nyumbani na ugenini ambapo mwenyeji atapanga tarehe ya mechi ambazo zinatakiwa kuchezwa kati ya Jumamosi au Jumapili. Mechi za marudiano katika raundi hiyo ya kwanza zitachezwa kati ya Mei 18 na 19 mwaka huu.

Katika upangaji huo ulioshuhudiwa na waandishi wa habari kwa niaba ya klabu husika, mabingwa wa Mkoa wa Shinyanga (Stand Ngaya FC) wamepita moja kwa moja hadi raundi ya pili itakayochezwa kati ya Mei 25 na 25 mwaka huu wakati mechi za marudiano ni kati ya Juni 1 na 2 mwaka huu.

Raundi ya tatu itachezwa kati ya Juni 8 na 9 mwaka huu wakati marudiano ni Juni 15 au 16 mwaka huu. Raundi ya nne itachezwa kati ya Juni 22 au 23 mwaka huu wakati marudiano ni Juni 29 au 30 mwaka huu. Raundi ya tano ni kati ya Julai 6 na 7 mwaka huu na marudiano ni Julai 13 au 14 mwaka huu.

Timu tatu ndizo zitakazopanda kucheza Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu ujao, ambazo ni ya kwanza nay a pili wakati timu ya tatu itapatikana kwa timu zilizoshindwa hatua ya nusu fainali kucheza zenyewe kwa zenyewe. Washindi wa nusu fainali nao watacheza wenyewe kwa wenyewe ili kupata bingwa wa RCL ambaye atakabidhiwa kombe la ubingwa.

Ligi hiyo inashirikisha mabingwa kutoka mikoa 27 ya kimpira ambapo katika raundi ya kwanza wanaanza mabingwa 26, raundi ya pili ni mabingwa 14 wakijumuisha na bingwa wa Shinyanga ambaye katika draw ameingia moja kwa moja katika hatua hiyo.

Raundi ya tatu itashirikisha timu saba zilizosonga mbele pamoja na moja yenye uwiano mzuri wa matokeo ili kufanya jumla ya timu nane. Raundi ya nne itakuwa na timu nne. Wakati raundi ya tano itakuwa ni kumpata bingwa na mshindi wa tatu.

Katika upangaji huo wa ratiba mechi za raundi ya kwanza (timu ya kwanza ikianzia nyumbani) itakuwa kama ifuatavyo; Red Coast vs Abajalo, Kariakoo vs Mtwara, Friends Rangers vs Kiluvya United,  TECKFOLT FC vs African Sports, Machava FC vs Flamingo SC, Gunners United vs Manyara na Simiyu vs Magic Pressure FC.

Nyingine ni Polisi Jamii Bunda FC vs UDC FC, Geita vs Biharamulo SC, Saigoni SC vs Tabora, Katavi Warriors vs Rukwa United, Mji Njombe vs Mbinga United na Kimondo FC vs Iringa.

Mechi zitachezwa katika viwanja vya makao makuu ya mikoa, vinginevyo kuwepo na maombi rasmi ambayo yatakubaliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

SIMBA, MGAMBO SHOOTING UWANJANI KESHO
Timu za Simba na Mgambo Shooting ya Tanga zinaumana kesho (Mei 8 mwaka huu) katika mchezo pekee wa Ligi Kuu ya Vodacom utakaofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Viingilio katika mechi hiyo itakayoanza saa 10.30 jioni vitakuwa sh. 5,000 kwa viti vya bluu na kijani, sh. 8,000 viti vya rangi ya chungwa, sh. 15,000 kwa VIP C na B wakati VIP A ni sh. 20,000.

RUVU SHOOTING, SIMBA ZAINGIZA MIL 17
Mechi namba 111 ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Ruvu Shooting na Simba iliyochezwa juzi (Mei 5 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa Simba kushinda mabao 3-1 imeingiza sh. 17,700,000.

Watazamaji 3,163 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo ambayo viingilio vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 3,485,752.45 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 2,700,000.

Kiingilio cha sh. 5,000 ndicho kilichovutia watazamaji wengi ambapo waliokata tiketi hizo walikuwa 2,901 na kuingiza sh. 14,505,000 wakati idadi ndogo ya washabiki ilikuwa ya kiingilio cha sh. 20,000 kilichovutia washabiki 28 na kuingiza sh. 560,000.

Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 1,772,416.50, tiketi sh. 3,183,890, gharama za mechi sh. 1,063,449.90, Kamati ya Ligi sh. 1,063,449.90, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 531,724.95, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 206,781.93 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA) sh. 206,781.93.

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

0 comments:

Post a Comment