Profesa Lipumba alisema hiyo inatokana na wasiwasi
kuwa mchakato wa Katiba Mpya hautaweza kukamilika mwaka 2014 hivyo
kutokuwa rahisi kwa uchaguzi kufanyika mwaka 2015.
Akizungumza Dar es Salaam jana, wakati akifungua
kikao cha Baraza Kuu la CUF, Profesa Lipumba alisema kuwa Serikali
inataka kuongezewa muda wa kukaa madarakani kwa miaka miwili ikimaanisha
kuwa Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Rais Jakaya Kikwete itakaa
madarakani hadi mwaka 2017.
Hata hivyo, madai hayo ya Profesa Lipumba
yamepingwa vikali na Serikali na viongozi wake watatu waandamizi ambapo
walijibu walipoulizwa kwa maandishi na mwandishi wetu mjini Dodoma
wanakohudhuria kikao cha Bunge.
Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe
alijibu: “Mchakato wa Katiba upo ‘on track’ (unakwenda vizuri) hatuna
sababu ya kufanya hivyo.”
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema alijibu” “Njooni ofisini kwangu nitasema ni kitu gani.”
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera,
Uratibu na Bunge, William Lukuvi alijibu kwa utani bila ya kufafanua:
“Njooni niwajuze, unajua kamba haitoki Ukambani kama ilivyo kamba.”
Profesa Lipumba amemwomba Rais Kikwete asilikubali
wazo hilo akisema wananchi hawatakubali na taifa linaweza kuingia
katika mtafaruku.
“Nitapenda kuona Rais Kikwete akikataa jambo hilo
kwani litachafua taswira ya nchi. Hatua hii ni kinyume cha utawala
bora,” alisema Profesa Lipumba.
Alisema Serikali haipaswi kuhofia uchaguzi kwa
sababu ya Katiba kwani bado uwezekano wa kuandaa uchaguzi wa haki na
huru unawezekana kwa utaratibu mwingine.
“Mchakato wa Katiba unaendelea, Tume ya Mabadiliko
ya Katiba inatuambia kwamba mwaka 2014 tutakuwa na Katiba Mpya, sasa
CUF tunasema kwamba hata kama Katiba Mpya haitapatikana kwa kipindi
hicho kuwe na Tume huru ya Uchaguzi,” alisema Profesa Lipumba.
Jukwaa la Katiba kutinga mahakamani
Siku nne baada ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kutoa rasimu ya
mwongozo kuhusu uundwaji wa Mabaraza ya Katiba, Jukwaa la Katiba
Tanzania (Jukata), limesema litafungua kesi mahakamani kutaka kusitishwa
kwa mchakato mzima wa Katiba Mpya kwa madai kuwa uendeshwaji wake
umejaa mizengwe, itikadi za vyama na rushwa. Limetaja sababu tano ambazo
zimekiukwa.
Limesema kesi hiyo itasimamiwa na timu ya mawakili
10 watakaoongozwa na Mwanasheria wa masuala ya Haki za Binadamu, Dk
Rugemeleza Nshala na itawasilishwa mahakamani siku saba zijazo kuanzia
jana.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam
jana, Mwenyekiti wa Jukata, Deus Kibamba alitaja sababu hizo kuwa ni
kutokufanyiwa marekebisho katika sehemu tatu za Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba kama ilivyoahidiwa na Rais Kikwete, kuvurugwa kwa Uchaguzi wa
Mabaraza ya Katiba, mchakato wa Katiba kukosa uongozi, kuminywa kwa
demokrasia wakati wa mchakato huo pamoja na Jukwaa hilo kuzuiwa kuonana
na Rais ili kueleza upungufu uliopo.
chanzo mwananchi.
chanzo mwananchi.
0 comments:
Post a Comment