SIMBA YAINGIZA MIL 134/-, AZAM MIL 34/-
PAMBANO
la Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Simba na Libolo FC ya Angola
lililofanyika jana (Februari 17 mwaka huu) limeingiza sh. 133,795,000
wakati lile la Kombe la Shirikisho kati ya Azam na El Nasir ya Sudan
Kusini lililochezwa juzi (Februari 16 mwaka huu) limeingiza sh.
34,046,000.
Watazamaji
22,469 walikata tiketi kushuhudia mechi ya Simba kwa viingilio vya sh.
5,000, sh. 10,000, sh. 15,000, sh. 20,000 na sh. 30,000. Simba ilipoteza
pambano hilo kwa bao 1-0.
Mgawo
wa mechi hiyo ulikuwa kama ifuatavyo; gharama za waamuzi sh.
24,926,500, gharama za tiketi sh. 7,410,000, asilimia 15 ya uwanja baada
ya kuondoa gharama za waamuzi na tiketi ilikuwa sh. 15,218,775,
asilimia 10 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Shirikisho
la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) sh. 10,145,850 na asilimia 75
iliyokwenda klabu ya Simba ni sh. 76,093,875.
Mechi
ya Azam iliyomalizika kwa wenyeji kuibuka na ushindi wa mabao 3-1
ilishuhudiwa na watazamaji 13,431 kwa viingilio vya sh. 2,000, sh.
5,000, sh. 10,000 na sh. 20,000. Mgawo katika mechi hiyo ulikuwa kama
ifuatavyo;
Gharama
za tiketi sh. 4,779,000, asilimia 15 ya uwanja baada ya kuondoa gharama
za tiketi ilikuwa sh. 4,390,050, asilimia 10 ya Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF) na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) sh.
2,926,700 na asilimia 75 iliyokwenda Prime Time Promotions (Azam) ni sh.
29,267,00.
PONGEZI KWA UONGOZI MPYA SPUTANZA, FRAT
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa pongezi kwa uongozi mpya wa
Chama cha Wachezaji Mpira wa Miguu Tanzania (SPUTANZA) na wa Chama cha
Waamuzi wa Mpira wa Miguu Tanzania (FRAT) uliochaguliwa wiki iliyopita.
Uongozi
wa FRAT ulichaguliwa Februari 13 mwaka huu mjini Morogoro wakati wa
SPUTANZA ulichaguliwa jana (Februari 17 mwaka huu) katika uchaguzi
uliofanyika Kigamboni, Dar es Salaam.
Waliochaguliwa
kuongoza SPUTANZA na hawakuwa na wapinzani ni Musa Kissoky (Mwenyekiti)
na Said George (Katibu Mkuu) wakati Ali Mayai aliwashinda Isaac
Mwakatika na Hakim Byemba katika nafasi ya mjumbe wa Mkutano Mkuu wa
TFF.
Kusianga
Kiata na Charles Mngodo walichaguliwa kuwa wajumbe wa Kamati ya
Utendaji ya SPUTANZA. Katika uchaguzi huo uliohudhuriwa na wapiga kura
17, Mhazini na nafasi moja ya mjumbe wa Kamati ya Utendaji zitajazwa
baadaye kutokana na kukosa wagombea.
Kwa
upande wa FRAT viongozi waliochaguliwa ni Said Nassoro (Mwenyekiti),
Charles Ndagala (Katibu Mkuu) na Kamwanga Tambwe (mjumbe wa Mkutano Mkuu
wa TFF).
Ushindi
waliopata viongozi waliochaguliwa kuongoza vyama hivyo unaonesha jinsi
wapiga kura walivyo na imani kubwa kwao, na TFF inaahidi kuendeleza
ushirikiano wake kwa Kamati ya Utendaji ya FRAT na SPUTANZA.
Uongozi
huo mpya una changamoto nyingi, kubwa ikiwa ni kuhakikisha unaendesha
shughuli za mpira wa miguu kwa kuzingatia katiba zao pamoja na vyombo
vya mpira wa miguu vilivyo juu yao.
Pia
tunatoa pongezi kwa kamati za uchaguzi za FRAT na SPUTANZA na Kamati ya
Uchaguzi ya TFF kwa kuhakikisha uchaguzi umeendeshwa kwa mujibu wa
Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
0 comments:
Post a Comment