Muda mchache baada ya Rais Mohammed Mursi
kulihutubia taifa kwa njia ya televisheni na kusema kwamba
hatojiuzulu kukidhi matakwa ya waandamanaji na jeshi,
uongozi wa juu wa kijeshi nchini humo umesema kwamba
uko tayari kufa katika kuwalinda watu wa Misri dhidi ya wale
waliowaita "magaidi na wapumbavu."
Taarifa iliyotumwa kwenye ukurasa wa Facebook wa Baraza
Kuu la Kijeshi, linaloongozwa na mkuu wa majeshi, Jenerali
Abdel Fattah al-Sisi, inasomeka: "Tunaapa kwa Mungu
kwamba tutajitolea muhanga hata damu yetu dhidi ya gaidi,
mtu mwenye siasa kali au mpumbavu yeyote."
Tamko hili limetolewa masaa matatu tu tangu Mursi kukataa
sharti lililotolewa na al-Sisi ambalo lilimtaka rais huyo
kugawana madaraka na wapinzani wake au akabiliwe na
suluhisho la kijeshi kufikia saa 11 jioni.
Chanzo kimoja cha kijeshi kimesema kwamba taarifa hiyo
inaweka wazi kwamba jeshi halitaachana na madai yake.
Katika hotuba yake ya usiku wa kuamkia leo, Mursi
aliwaalika wapinzani kujiunga na majadiliano, lakini
wapinzani wamekuwa wakikataa mara kwa mara
mazungumzo hayo.
Wakati hayo yakitokea, taarifa za hivi punde zinasema
kwamba makabiliano kati ya wafuasi wa Mursi na vikosi vya
usalama yamesababisha watu 16 kuuawa na zaidi ya 200
kujeruhiwa.
Mashahidi wanasema wamesikia milio ya risasi karibu na
Chuo Kikuu cha Cairo, ambako wafuasi hao walikusanyika
kumuunga mkono kiongozi wao.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment