Kukiwa na sintofahamu kuhusu mustakabali wa kocha wa Real
Madrid Carlo Ancelotti katika klabu hiyo, wachezaji na mashabiki wa timu hiyo
wameonekana kumhitaji kocha huyo kwa msimu ujao wa Ligi kuu ya soka nchini
Hispania na mashindano mengine.
Miongoni wa wachezaji wanaoonekana kumuunga mkono kocha
huyo ni mshambuliaji wa timu hiyo Cristiano Ronaldo.
Baada ya mchezo wa Ligi hapo jana kati ya Real Madrid na
Getafe, Ronaldo aliandika katika mtandao wa kijamii wa Twitter akisema kuwa ana
imani wataendelea kuwa na kocha huyo msimu ujao.
Mashabiki wa Real Madrid nao hawakuwa nyuma katika hilo
kwani walikuwa wakiimba jina la kocha huyo katika mchezo huo hapo jana.
Lakini taarifa kutoka timu ya Ac Milan ya nchini Italia
zinasema kuwa mmilikiwa wa klabu hiyo Silvio Berlusconi yupo tayari kumrudisha
kocha huyo katika klabu ya Ac Milan endapo Real Madrid watamfungashia virago
vyake.
Katika kuonesha kuwa Milan wamepania kumrudisha kocha
huyo aliyewahi kuifundisha timu hiyo kwa muda wa miaka nane, timu hiyo
imemtengea kocha huyo kiasi cha euro milioni 150 za usajili.
Carlo Ancelotti kwa upande wake anasema kuwa atakuwa na
mapumziko ya kufundisha endapo Real Madrid wataamua kuachana naye.
0 comments:
Post a Comment