WANG’AMUZI
VIPAJI MABORESHO STARS WAJICHIMBIA LUSHOTO
Wang’amuzi vipaji 28 wanakutana Lushoto mkoani
Tanga kwa siku saba katika mpango maalumu wa maboresho ya Taifa Stars ambapo
watatoka na orodha ya mwisho ya wachezaji waliopatikana katika mechi za
maboresho hayo zilizochezwa nchi nzima.
Katika kikao hicho, wang’amuzi hao watapitia majina
ya wachezaji walioteuliwa ikiwemo kuwaangalia tena kwenye video kwa vile mechi
zote zilirekodiwa. Wachezaji watakaoteuliwa katika mpango huo baadaye wataingia
kambini mkoani Mbeya.
Wang’amuzi vipaji ambao wanaoondoka Machi 9 mwaka
huu kwenda Lushoto ni Abdul Mingange, Boniface Pawasa, Charles Mkwassa, Dan
Korosso, Dk. Mshindo Msolla, Edward Hiza, Elly Mzozo, Hafidh Badru, Hamimu
Mawazo, John Simkoko, Jonas Tiboroha, Juma Mgunda na Juma Mwambusi.
Kanali mstaafu Idd Kipingu, Kenny Mwaisabula, Madaraka
Bendera, Madaraka Selemani, Mbarouk Nyenga, Mohamed Ally, Mussa Kissoky, Nicholas
Mihayo, Peter Mhina, Salum Mayanga, Salvatory Edward, Sebastian Nkoma, Sekilojo
Chambua, Selemani Jabir na Shabani Ramadhan.
Wengine ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF
ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi, Kidao Wilfred, Mjumbe wa Kamati
ya Utendaji ya TFF ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Vijana, Ayoub Nyenzi,
Kaimu Mkurugenzi wa Ufundi, Salum Madadi na Mshauri wa Rais (Ufundi),
Pelegrinius Rutayuga.
MUJUNI
KUICHEZESHA AFC LEOPARDS CC
Mwamuzi
Israel Mujuni ameteuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu (CAF) kuchezesha mechi
ya marudiano ya Kombe la Shirikisho (CC) Afrika kati ya wenyeji AFC Leopards ys
Kenya na SuperSport United ya Afrika Kusini.
Mujuni
katika mechi hiyo itakayochezwa kesho (Machi 8 mwaka huu) jijini Nairobi, Kenya
atasaidiwa na Samuel Mpenzu, Josepht Bulali wakati mwamuzi wa mezani atakuwa
Ramadhan Ibada.
Kamishna
wa mechi hiyo ni Amir Hassan kutoka Mogadishu, Somalia. SuperSport United
ilishinda mechi ya kwanza iliyochezwa wiki mbili zilizopita mabao 2-0.
SIMBA YALIMWA
FAINI KWA KUENDEKEZA VITENDO VYA KUSHIRIKINA
Bodi
ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imeipiga faini ya jumla ya sh. milioni moja klabu
ya Simba kutokana na makosa mbalimbali ikiwemo vitendo vinavyoashiria
ushirikina uwanjani.
Simba
ilifanya vitendo hivyo katika mechi yake dhidi ya Mbeya City ambapo imepigwa
faini ya sh. 500,000. Pia imepigwa faini nyingine ya sh. 500,000 kwa makocha
wake Loga, Selemani Matola na Idd Pazi kuingia uwanjani na kumzonga mwamuzi
kwenye mechi hiyo.
Naye
mshambuliaji wa Simba, Amisi Tambwe amepigwa faini ya sh. 500,000 kwa
kushangilia bao alilofunga kwenye mechi hiyo kwa kuonesha ishara ya matusi kwa
kidole.
Mbeya
City imepigwa faini ya sh. 300,000 kwa washabiki wake kuingia uwanjani kwenye
mechi dhidi ya Kagera Sugar iliyochezwa mjini Bukoba. Klabu za Yanga na Coastal
Union zimepigwa faini ya sh. 500,000 kila moja kwa washabiki wao kurusha chupa
za maji uwanjani wakati timu hizo zilipopambana jijini Tanga.
Kiungo
wa Mtibwa Sugar, Shabani Nditi amepigwa faini ya sh. 500,000 kwa kumpiga
mchezaji wa Simba, wakati Salvatory Ntebe pia wa Mtibwa Sugar amepigwa faini ya
sh. 500,000 kwa kumtukana refa kwenye mechi dhidi ya Mbeya City.
Pia
mshambuliaji wa Mtibwa Sugar, Musa Mgosi amepigwa faini ya sh. 500,000 kwa kosa
la kupiga uwanjani kwenye mechi dhidi ya Ashanti United ambapo vilevile atakosa
mechi tatu za ligi. Coastal Union imepigwa faini ya sh. 500,000 kwa washabiki
wake kumrushia chupa za maji kipa wa Mbeya City.
Nayo
JKT Ruvu imepigwa faini ya sh. 300,000 kwa kuchelewa kufika uwanjani kwenye
mechi dhidi ya Simba iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Vilevile
wamiliki wa Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga wameandikiwa barua ya kufanya
marekebisho ya vyumba vya wachezaji, kwa vile havina hewa ya kutosha.
Kwa
upande wa Ligi Daraja la Kwanza (FDL) klabu zilizopigwa faini kutokana na
makosa mbalimbali ni Friends Rangers (sh. 200,000), Lipuli (sh. 200,000), Majimaji
(sh. 400,000), Polisi Morogoro (sh. 400,000) na Transit Camp (sh. 200,000).
Kocha
Msaidizi wa Polisi Morogoro, John Tamba atapelekwa kwenye Kamati ya Maadili
kutokana na vitendo visivyo vya kimaadili katika mechi dhidi ya Burkina Faso.
Kiongozi
wa Lipuli, Hamis Kiemba na wachezaji Boniface Sawaka, George Enock na Green Paul
watapelekwa katika Kamati ya Nidhamu kutokana na utovu wa nidhamu waliofanya
kwenye mechi dhidi ya Kimondo.
Naye
mchezaji Sangalau Nyamoka wa JKT Kanembwa aliyelalamikiwa uhalali wake na
Polisi Tabora suala lake linapelekwa Kamati ya Nidhamu.
COASTAL,
ASHANTI KUUMANA MKWAKWANI VPL
Ligi
Kuu ya Vodacom (VPL) inaendelea kesho (Machi 8 mwaka huu) kwa mechi tatu ambapo
Coastal Union itaumana na Ashanti United kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini
Tanga.
Ruvu
Shooting itaikaribisha Oljoro JKT kwenye Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani
Pwania wakati Mbeya City itacheza na Rhino Rangers kwenye Uwanja wa Kumbukumbu
ya Sokoine jijini Mbeya.
Mechi
za Jumapili (Machi 9 mwaka huu) ni Tanzania Prisons na Simba kwenye Uwanja wa
Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya, na JKT Ruvu na Mtibwa Sugar zitacheza
Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi, Dar es Salaam.
FDL
KUTIMUA VUMBI WIKIENDI
Ligi Daraja la Kwanza (FDL) inaendelea
wikiendi hii kwa timu za makundi yote matatu kushuka kwenye viwanja tofauti
nchini ambapo kesho (Machi 8 mwaka huu) Tessema itacheza na Transit Camp kwenye
Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.
Kundi B ni Burkina Faso vs Kurugenzi
(Jamhuri, Morogoro) wakati C Polisi Tabora vs Mwadui (Ali Hassan Mwinyi), Stand
United vs Pamba (Kambarage), Polisi Mara vs Kanembwa JKT (Karume) na Polisi
Dodoma vs Toto Africans (Jamhuri, Morogoro).
Mechi za Jumapili ni kundi A, African
Lyon vs Polisi Dar (Karume), Villa Squad vs Friends Rangers (Mabatini, Pwani)
na Ndanda vs Green Warriors (Nangwanda Sijaona, Mtwara). Kundi B ni Polisi
Morogoro vs Majimaji (Jamhuri, Morogoro) na Mlale JKT vs Lipuli (Majimaji,
Songea).
Boniface Wambura Mgoyo
Media and Communications Officer
Tanzania Football Federation (TFF)
0 comments:
Post a Comment