Main Menu

Monday, December 23, 2013

WAWANAKE MKOANI IRINGA WATAKIWA KUZITAMBUA HAKI ZAO.


WAWANAKE mkoani Iringa wametakiwa kuzitambua haki zao sambamba na sheria za utawala bora ndani ya jamii katika kukabiliana na changamoto mbalimbali katika masuala ya utawala na mifumo ya maisha ihusuyo tamaduni mbalimbali zinachochangia kuchochea vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia dhidi yao.

Hayo amesema Mkuu wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Ruaha (RUCO) Dk. Cephas Mgimwa wakati wa mafunzo ya juu ya haki za wanawake yaliyoandaliwa na Kitengo cha Haki za Binadamu na Utawala bora wa chuo hicho kwa wanawake wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa yaliyofanyika katika ukumbi mdogo wa chuoni hapo.

Amesema kuwa wanamke anapaswa kupewa nafasi za kutoa michango yao katika maamuzi mbalimbali ndani ya jamii ikiwemo masuala ya ndoa, umiliki wa mali na masuala ya mirathi.

Amesema mafunzo hayo ya utawala bora yamelenga kuwajengea uwezo wanawake kufikia mifumo mbalimbali ya mahakama ili kupata msaada wa kisheria kwa lengo la kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazowakabili wanawake zikiwemo kupigwa, kubakwa, kuachika (talaka) na kunyimwa mirathi kutokana na baadhi ya mila potofu katika baadhi ya makabila.

Mgimwa amesema kumekuwa na unyanyasaji wa kijinsia katika jamii nyingi za Kitanzania hasa watoto na wanawake walioko ndani ya ndoa na nje ya ndoa na kwa kukosa ufahamu wa sheria na haki za binadamu wengi wao wameshindwa kupeleka malalamiko yao sehemu husika.

Kwa upande wake Mhadhiri na Mkuu wa Kitengo cha Sheria wa chuo hicho Dk. Mary Livera amesema binadamu wote ni sawa na hakuna tofauti ya mwanamke na mwanaume katika kupata haki za msingi za binadamu kila mmoja anastahili kupata haki katika huduma za mifumo ya sheria katika mahakama.


0 comments:

Post a Comment